Baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakochezwa leo kati ya Yanga SC na KMC FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam utafungwa kwa mwezi mmoja kupisha marekebisho hasa kwenye eneo la kuchezea.
Meneja wa uwanja huo Salum Mtumbuka amesema kuwa baada ya michezo miwili ya mashindano ya Afrika mwishoni mwa wiki walikutana na maafisa wa Shirikisho la Soka Afrika ambao waliwapa maelekezo ya kufanya marekebisho hayo.
“Tulikubaliana na CAF wakati marekebisho yanaendelea, mechi zitakazochezwa hapo labda zile za kimataifa za CAF na timu ya Taifa. Mechi nyingine za ligi kuu watatumia Uwanja wa Uhuru au viwanja vingine,” amesema Mtumbuka
Aliongeza kuwa ndani ya wiki moja uwanja unatakiwa kutumika kwa mechi tatu, lakini kati ya Jumamosi na leo uwanja huo utakuwa umetumika mara nne.
Hata hivyo, licha ya uwanja huo kufungwa, mchezo wa ligi utakaoathirika ni mmoja ambapo Yanga walitarajiwa kuutumia kuikaribisha Geita Gold Machi 12 mwaka huu.
Mechi ambazo zitachezwa hapo marekebisho yakiendelea ni Machi 7 na Machi 17 ambapo Simba SC itaikaribisha Vipers na Horoya mtawalia, na pia wakati Yanga itakapoikaribisha Real Bamako na US Monastir, Machi 8 na Machi 19, mtawalia.