Niko tayari kwa mdahalo na Trump

0
136

Rais wa Marekani, Joe Biden amesema “atafurahi” kukabiliana na Donald Trump katika mdahalo kabla ya uchaguzi mkuu wa Novemba.

Biden alikuwa akijibu swali la Howard Stern wakati wa mahojiano ya saa moja kwenye mtandao wa redio ya satelaiti ya SiriusXM.

“Nitakuwa na furaha kufanya naye mdahalo,” amesema na kuongeza hata hivyo kwamba hajajua itakuwa lini.

Kufuatia kauli hiyo, mshauri wa kampeni wa Trump, Chis LaCivita alijibu kwenye X/Twitter: “Sawa, ngoja tujipange!”

Kwa asili, midahalo ya urais katika mwaka wa uchaguzi huwa inaandaliwa na tume isiyoegemea upande wowote na kupangwa kufanyika siku chache kabla ya uchaguzi.

Novemba mwaka jana tume hiyo ilitangaza maeneo matatu ya wagombea urais 2024 kufanyia midahalo – katika vyuo vikuu vya Texas, Utah na Virginia – na ikapendekezwa iwe kati ya Septemba na Oktoba.

Kabla ya matamshi yake ya sasa, Biden hakuonekana kuhitaji kufanya mdahalo na Trump . Katika kauli yake ya mwezi Machi alisema kupanda jukwaani kwa ajili ya mjadala na Trump “kutategemea tabia yake”.