Watoa ushauri kuepuka athari za mafuriko

0
152

Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, shirika la kutoa misaada kwenye majanga la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limetoa ushauri kwa watu ili kuepuka au kupunguza madhara ya mafuriko.

Maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko nchini Kenya ni Ukanda wa Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Kusini Mashariki, Pwani, Kaskazini Mashariki na Jiji la Nairobi.

Msalaba Mwekundu (Red Cross) wamewataka watu wanaoishi mabondeni kuhamia maeneo ya juu ili waepuke kusombwa na maji endapo mafuriko yatatokea.

Wakati panapotokea mafuriko na kuingia ndani ya nyumba, shirika hilo limeelekeza watu kuzima umeme kwenye swichi kuu ili kuepuka hatari zaidi.

Lingine ambalo Wakenya wametahadharishwa ni kuepuka kutembea kwenye maji yanayotiririka kwa kasi.

“Hata maji ya kina cha inchi sita yanaweza kikuangusha na kukuzoa… Futi moja ya maji yanayotembea pia yanaweza kusomba gari,” imeeleza taarifa ya shirika hilo.

Waendeshaji magari pia wamekanywa wasipite kwenye madaraja yaliyofunikwa na maji, bali wasubiri daraja lionekane kwa usahihi.

Vile vile Msalaba Mwekundu wamewataka watu kupima kina cha maji kwa kijiti kabla ya kupita maeneo yaliyofurika.

Shirika pia limetahadharisha watu kutosogelea nguzo za umeme zilizosombwa au kuangushwa na maji sambamba na kuepuka kukaa chini ya nyaya za umeme mvua zinapokuwa zinanyesha.

Chanzo: Taifa Leo