Mawaziri wa SADC waipa pole Tanzania

0
241

Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaendelea na mkutano wake jijini Luanda, Angola ambapo katika siku ya kwanza ya mkutano huo limewasilisha salamu za rambirambi kwa Tanzania kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia Februari 29, 2024.

Salamu hizo zimewasilishwa naMwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola
Balozi Tete António pamoja na Mawaziri wengine wa nchi za SADC.

Wakitoa salamu hizo za pole, Mawaziri hao wamesifu uongozi mahiri na mchango wa Hayati Mzee Mwinyi katika maendeleo ya Tanzania na SADC hasa alipokuwa Mwenyekiti wa lililokuwa Jukwaa la uratibu wa masuala ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADCC) mwaka 1989 hadi 1990 na kuongoza mchakato wa kubadili Jukwaa hilo kuwa SADC.

Kwa muda wa siku mbili Baraza hilo la Mawaziri la SADC pamoja na mambo mengine linapitia, kujadili na kuridhia bajeti ya SADC kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.