‘GOOGLE TIMELAPSE’ YAREKODI MWONEKANO WA DUNIA 2020-2022

0
1200

Kampuni ya kiteknolojia ya Google imeachilia kipengele kipya ‘update’ cha mfumo wa kuhesabu muda ulimwenguni wa ‘Google Timelapse’ ya miaka miwili kuonesha namna dunia imekuwa ikipitia mabadiliko mbalimbali ikiwemo ya tabianchi na kukua kwa miji.

Aina hii ya mfumo wa kuhesabu muda ni kipengele kinachomwezesha mtu kujionea namna Sayari ya dunia imebadilika kwa wakati husika ambapo hapo awali Google Timelapse iliachiliwa ya kuanzia mwaka 1984 hadi 2020 na sasa kipengele hicho kipya kinaongezea miaka miwili 2020 hadi 2022.

Hii ina maana kwamba watumiaji wa mfumo huo sasa wanaweza kuona namna ulimwengu umepitia mabadiliko katika kipindi cha miaka miwili ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, ukuaji wa miji kwa namna miji hiyo ilivyo stawi, kuyayuka kwa barafu katika milima na majanga ya asili kuonesha namna misitu ilivyoharibiwa na majanga mengine kama mmomonyoko wa udongo kutokana na mafuriko na shughuli za kibinadamu.

Watafiti wanaweza kutumia njia hiyo kuyasoma mabadiliko ya hali ya hewa na athari za shughuli za wanadamu kwenye sayari ya dunia huku wengine wakitengeneza video za muda mfupi zikionesha mwonekano na kulinganisha maeneo mbalimbali ya duniani kwa vipindi vya nyuma na vipindi vya sasa.