Ujenzi wa nyumba za tope wamkera Byakanwa

0
531

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, – Gelasius Byakanwa ameendelea kuonesha kuchukizwa na ujenzi wa nyumba za tope unaoendelea kwenye baadhi ya maeneo ya mkoa huo huku akisisitiza kuwa ni lazima ujenzi huo ukomeshwe.

Byakanwa amezungumza hayo alipokuwa akitoa salamu za sikukuu ya Krismasi za mkoa wa Mtwara katika kanisa la Biblia Tanzania ilipofanyika Ibada ya kitaifa ya Krismasi kwa mwaka huu.

“Wakati wa kifo nyie wachungaji na maaskofu mkituzika mnatuambia ulitoka mavumbini na mavumbini utarudi, sasa tumetathmini kuna watu wao wanaishi kwenye nyumba za udongo halafu nyumba hiyo imeezekwa kwa majani nayo yameoza, kipindi cha mvua anahama kupisha mvua, huyo anaishi mavumbini siku zote za maisha yake,”amesema Byakanwa.

Ameongeza kuwa suala la kuishi mahali pazuri sio kipimo cha mafanikio na pia ni muhimu kwa mkazi wa Mtwara kuonesha kuchukizwa na makazi ya nyumba za tope.

“Mimi nataka nikwambie sijafanikiwa na sioni kama nimefanikiwa, napambana kuona kama nitafanikiwa kwa nini wewe hupambani kufanikiwa, na mimi ninao ndugu zangu wanaishi katika nyumba za mavumbi nao ujumbe huu uwafikie,”amesema Mkuu huyo wa mkoa wa Mtwara.

Uongozi wa mkoa wa Mtwara, upo katika kampeni maalum ya kuhakikisha Wakazi wake wanaondokana na ujenzi wa nyumba za tope na wanaongeza kipato chao kwa kuzalisha mazao ya kibiashara.