Marekani kufungua Ubalozi mdogo Sahara Magharibi

0
320

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, -Mike Pompeo amesema nchi hiyo imeanza taratibu kwa ajili ya kufungua ubalozi mdogo huko Sahara Magharibi.

Waziri Pompeo amekuwa afisa wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka nchini Marekani kufanya ziara nchini Morocco tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia madarakani mwaka 2016.

Marekani imeweka wazi mpango huo zikiwa zimepita wiki chache baada ya utawala wa Rais Trump kutambua rasmi madai ya Morocco ya kumiliki koloni hilo la zamani la Hispania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Pompeo, ubalozi huo mdogo wa Sahara Magharibi utasimamiwa na ubalozi wa Marekani nchini Morocco.

Morocco ilichukua udhibiti wa jimbo la Sahara Magharibi lenye utajiri mkubwa wa madini mwaka 1975 baada ya mtawala wa kikoloni wa Hispania kujiondoa na kusababisha mapigano kwa ajili ya kudai Uhuru ambayo yalimalizika mwaka 1991 baada ya Umoja wa Mataifa kufanya usuluhishi na kupeleka askari wa kulinda amani katika eneo hilo.