UEFA yaichunguza Man City

0
872

Klabu ya Manchester City inachunguzwa kwa kukiuka kanuni za matumizi ya pesa kwenye usajili na uendeshaji wa klabu hiyo kupita kiasi ambacho klabu hiyo inaingizia kwenye mapato yake.

Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limesema kuwa linaendesha uchunguzi huo kufuatia siku za hivi karibuni kuchapishwa kwa nyaraka mbalimbali na vyombo vya habari, zinazoonyesha kuwa klabu hiyo ilidanganya kwenye taarifa yake kwa UEFA kuwa haikiuki misingi hiyo.

Pamoja na Manchester City kukanusha tuhuma hizo, UEFA imesema kuwa inaendesha uchunguzi huo ili kujua undani wake ambapo Manchester City inadaiwa kuficha matumizi ya kiasi cha Pauni Milioni 9.9 huku pia ikidaiwa kumlipa Pauni Laki Mbili kinyume cha  sheria Wakala wa aliyekuwa mchezaji wao Jadon Sancho alipokuwa na umri wa miaka 14 ili asalie kwenye klabu hiyo.

Hii ni mara ya pili kwa Manchester City kufanyiwa uchunguzi wa aina hiyo,  ambapo mwaka 2014 ilikutwa na hatia ya kutumia pesa nyingi kuliko inazoingiza na kutozwa faini ya Pauni Milioni 49 na kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji kwenye kikosi kilichoshiriki Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu wa 2014/2015.