Tanzania na Misri kushirikiana sekta ya uchukuzi

0
207

Waziri wa uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wizara yake imejipanga kuhakikisha inashirikiama na Wizara ya Uchukuzi ya Misri katika kuendeleza miradi yote iliyopangwa na Serikali kupitia wizara hiyo ili kuleta mafanikio makubwa zaidi nchini.

Waziri Mbarawa ameeleza hayo Jijini Dar es Salaam katika kikao kilichofanyika baina ya Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania na Wizara ya Uchukuzi ya Misri.

Waziri Mbarawa amemwelezea Waziri wa Uchukuzi wa Misri maeneo mbalimbali ya kuwekeza miradi nchini ikiwemo ujenzi wa gati kubwa katika Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa reli katika bandari za Mtwara na Tanga.

“Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika Sekta ya Uchukuzi kwa kusimamia ujenzi wa miundombinu nchini. Amehakikisha kuwa fedha nyingi imewekezwa katika miundombinu ya barabara, miundombinu ya viwanja vya ndege pamoja na miundombinu ya bandari,” amesema Mbarawa.

Pamoja na Mambo mengine, Profesa Mbarawa amemwomba Waziri wa Uchukuzi wa Misri kuridhia kuwapokea Watanzania kadhaa watakaokwenda kujifunza uendeshaji wa Mradi wa Reli ya Kisiasa (SGR).

“Ni wakati mzuri pia wa ushirikiano kati ya Chuo cha Baharia cha Tanzania (DMI) na Taasisi ya Mafunzo ya Ubaharia ya Misri kwani nchi hiyo ina uzoefu mkubwa na itapelekea kupatikana kwa mabaharia wenye uzoefu wa hali ya juu nchini kupitia chuo hicho,” amesema Waziri Mbarawa

(Imeandikwa na Happyness Hans)