Serikali kuweka taa kwenye barabara zote katika miji

0
213

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imesema itahakikisha inatenga bajeti ya kutosha ya kuweka taa katika barabara zote zinazopita katika miji ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi katika maeneo hayo. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa , mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba uliopo Wilaya ya Newala  mkoani Mtwara ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Rais Samia katika mikoa ya Kusini.

Aidha, Waziri Bashungwa amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaoendelea kutekeleza mradi wa barabara kuanzia Mnivata hadi Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami ili kazi iweze kukamilika na kwa viwango vya juu.

“Niwaombe wananchi wa Mtwara mtoe ushirikiano kwa wakandarasi na muwe sehemu ya miradi hii kwa upendo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameleta mabilioni ili tuweze kujenga lami kwa viwango vya juu”, – amesisitiza Bashungwa.