Majaliwa: Kifo cha Kwandikwa kimeacha pengo serikalini

0
171

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa kimeacha pengo serikalini na bungeni kwani marehemu alikuwa mchapakazi, mwadilifu na mtulivu katika utendaji kazi wake.

Amesema hayo leo akizungumza nyumbani kwa marehemu Kwandikwa, Kibaha Picha ya Ndege mkoani Pwani alipofika kutoa pole kwa familia.

“Mchango wake wa utendaji katika Serikali na bunge ni mkubwa sana. Alifanikiwa kuwavutia wengi kwa tabia yake ya upole, unyenyekevu na uzingatiaji wa taratibu na sheria za utumishi kila alipopangiwa kufanya kazi hivyo kifo chake ni pigo kwa taifa,” amesema Majaliwa.

Ameishukuru familia kwa kuridhia maombi ya kutaka mazishi yafanyike Jumatatu ijayo ili kuwapa nafasi waombolezaji wakiwemo wabunge kupata nafasi ya kusafiri kutoka waliko na kushiriki katika kutoa heshima za mwisho na mazishi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu leo amekwenda nyumbani kwa marehemu Biswad Msuya, kaka mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, kutoa pole kwa familia kufuatia kifo cha mpendwa wao.

Akizungumza na wafiwa na waombolezaji katika msiba huo Majaliwa amesema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha marehemu Biswad kwa mshtuko mkubwa na amewataka waombolezeji wamuombee mke wa marehemu na familia ili awape utulivu na uvumilivu wakati huu wa majonzi.