Ndama Mtoto wa Ng’ombe jela miaka 5

0
836

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wawili wakazi wa Kinondoni mkoani Dar es Salaam kulipa faini ya milioni 1.5 ama kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja.

Washitakiwa hao Shaban Ndama na Hussein Yusuph wamehukumiwa kulipa faini hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Issaya baada ya washitakiwa hao kufikia makubaliano na DPP kukiri mashitaka yanayowakabili.

Aidha, washitakiwa hao pia wametakiwa kulipa fidia ya dola za Marekani 150,000 ndani ya miezi minne, fedha walizojipatia kwa njia ya ulaghai kutoka kwa raia mmoja wa kigeni wakidanganya kumuuzia madini ya dhahabu 17kg wakati wakijua madini hayo sio halisi.

Awali akiwasomea washitakiwa hao maelezo ya kosa Wakili Komanya ameiambia mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati Januari 2020 na Agosti 2021 wilayani Kinondoni.

Hata hivyo baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya ameomba mahakama kuwapunguzia adhabu washitakiwa hao baada ya wao wenyewe kukiri kosa na kukubali kuanza kulipa kiasi hicho cha fedha ambapo wamefanikiwa kulipa dola za Marekani 50,000 ambazo mahakama imeridhia na kuwataka washitakiwa kukamilisha malipo ya fedha zilizobaki kama walivyokubaliana na DPP.

Mpaka Mwandishi wa TBC anaondoka mahakamani hapo washitakiwa walikuwa kwenye taratibu za kukamilisha malipo ya awali ili taratibu zingine za kimahakama ziweze kuchukua mkondo wake.

Emmanuel Samwel TBC