Wenger kurejea kibaruani Januari

0
1921

Aliyekuwa kocha wa washika mtutu wa jiji la London Arsenal, Mzee Arsene Wenger amesema kuwa anatarajia kurejea kibaruani kuanzia Januari Mosi mwaka 2019  na amepokea ofa kutoka kila kona ya dunia.

Mfaransa huyo mwenye  umri wa miaka 68 alisitisha huduma yake ya miaka 22 ndani ya kikosi cha Arsenal msimu uliopita na mpaka sasa bado hajajua kazi yake mpya itakuwa wapi ingawa amesema kufanya kazi na chama cha soka, timu ya taifa au kurejea Japan ambapo aliwahi kuifundisha timu ya Nagoya Grampus Eight,  mojawapo linawezekana.

Wenger amesema kuwa amepumzika vya kutosha, na sasa yupo tayari kufanya kazi tena  ingawa hajajua ni wapi na kuongeza kuwa miaka 22 aliyohudumu Arsenal imempa uzoefu wa kutosha na mezani kwake ana ofa za kutosha kutoka sehemu mbalimbali duniani,  hivyo ni yeye tu kuchagua wapi pa kwenda.

Wenger alianza kazi ya ukocha kwenye klabu ya Nancy  kabla ya kujiunga na Monaco ambapo alidumu nayo kwa miaka Saba na kushinda taji la Ufaransa katika msimu wa kwanza akiwa na timu hiyo na baadae kutimkia Japan ambapo alihudumu kwa muda mfupi kabla ya kujiunga na Arsenal mwaka 1996 na kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England, na saba ya kombe la FA.

Katika hatua nyingine,  Wenger amesema kuwa timu ya taifa ya Ujerumani bado inahitaji huduma ya kiungo Mesut Ozil ambaye alitangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya kukwaruzana na chama cha soka cha nchi hiyo siku chache baada ya kutolewa kwenye fainali za kombe la FIFA la dunia zilizofanyika nchini Russia.

Wenger ameongeza kuwa anaamini Ujerumani inamhitaji Ozil  na anategemea kocha wa timu hiyo Joachim Low  atamshawishi mchezaji huyo kurejea kwenye kikosi hicho kwani kiungo huyo ni mchezaji wa daraja la juu na siku zote anapenda kuona akicheza na asipochezea timu ya taifa kuna vitu atapoteza.