Man U na St-Germain kitanzini

0
902

Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limezitia hatiani timu za Manchester United na Paris St-Germain kufuatia vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyofanywa na mashabiki wa klabu hizo kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya uliochezwa Februari 12 mwaka huu kwenye dimba la Old Trafford.

Mashetani Wekundu Manchester United wenyewe wamekutwa na hatia ya mashabiki wake kurusha vitu mbalimbali uwanjani zikiwemo chupa za maji pamoja kuziba baadhi za njia huku PSG wakitiwa hatiani kwa makosa ya mashabiki wake kuwasha baruti za moto, kurusha chupa uwanjani, kuwabugudhi mashabiki wengine na kufanya fujo kwenye mitaa kabla ya mchezo.

Picha za baadhi ya matukio zinamuonesha winga wa zamani wa Manchester United ambaye kwa sasa anahudumu kwenye klabu ya PSG, – Angel Di Maria akirushiwa chupa ya maji na mashabiki wa United ingawa polisi wa uwanjani wamesema hawajamkamata mtu yoyote kuhusiana na matukio hayo na kwamba wamaendelea na uchunguzi.

Kesi dhidi ya mashitaka hayo itasikilizwa na kamati ya nidhamu na maadili ya UEFA Februari 28 mwaka huu.

Katika mchezo huo PSG waliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa Nunge dhidi ya United huku mabao ya matajiri hao wa Ufaransa yakifungwa kipindi cha pili na mlinzi Presnel Kimpembe katika dakika ya 53 na mshambuliaji  Kylian Mbappe aliyefunga bao la ushindi katika dakika ya 60.