Polisi kutoka nchi 14 kufanya mafunzo Tanzania

0
349

Jeshi la Polisi nchini linatarajia kuwa mwenyeji wa mafunzo ya utayari kwa vitendo (Field Training Exercise) kwa mwaka 2024 yatakayojumuisha nchi 14 wanachama wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), kati ya Aprili 13 – 18, 2024.

Akitoa tarifa hiyo leo Aprili 11, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime amesema mafunzo hayo ya pamoja yanatarajiwa kufanyika katika Shule ya Polisi Tanzania, Moshi ambapo takribani maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wapatao 670 watashiriki katika mafunzo hayo.

Misime amebainisha kuwa kufanyika kwa mazoezi hayo kunatokana na maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa EAPCCO katika mikutano yao ya kila mwaka.

Amezitaja nchi zinazotarajiwa kushiriki mbali na mwenyeji Tanzania kuwa ni Burundi, Eritrea, Djibouti, DRC Congo, Kenya, Comoros, Ethiopia, Visiwa vya Shelisheli, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudani Kusini na Uganda.

Msemaji huyo wa polisi amebainisha kuwa lengo la zoezi hilo na mengine yaliyopita ni kuwajengea maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali uwezo wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu unaovuka mipaka kama vile ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya dawa za kulevya pamoja na kubadilishana uzoefu na taarifa za kiintelejensia.