Msipime viwanja kwenye mkondo wa maji

0
135

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amefika Mlima Kawetele ulioporomoka alfajiri ya leo Aprili 14, 2024 na kusababisha kufukiwa kwa nyumba 20, Ng’ombe wanne na kuharibika kwa miundombinu ya shule ya Mary’s katika Mtaa wa Gombe Kata ya Itezi Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Akiwa katika eneo hilo Homera amekanusha uvumi unaozagaa mitandaoni kwamba kuna maafa katika tukio hilo na kuongeza kuwa zaidi ya madhara aliyoyataja hakuna madhara mengine.

Homera ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kufanya tathimini ya waathirika na kuhakikisha wale ambao hawana malazi kufuatia tukio hilo wanapatiwa malazi wakati huu ambao Serikali inaendelea kupambana kuhakikisha hali inarejea kama kawaida.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya pia amekiagiza Kitengo cha Ardhi Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuacha kuwapimia wananchi viwanja eneo lenye changamoto hasa ya Mkondo wa Maji kwani kufanya hivyo kunasababisha matatizo kama hayo ambayo yangeweza kuzuilika.