Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wana Diaspora wote kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kokote waliko, na wawe tayari kuainisha fursa zilizopo.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo Tokyo nchini Japan alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Tanzanite, ambayo ni Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Japan.
Amewataka watambue fursa zilizopo nchini na kuzisemea vizuri, ili iwe fursa ya kupata wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na ikibidi wafanye ubia na Watanzania.
“Ninyi ni mabalozi wetu, itangazeni Tanzania na onesheni fursa zilizopo nchini ili tupate wawekezaji mahiri wenye mitaji ya kuja kuwekeza nyumbani.” amesema Waziri Mkuu
Amewataka pia watumie lugha ya kiswahili kama njia ya kukuza ajira, kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka kwenye mitaala yao.
Jumuiya hiyo ya Watanzania wanaoishi Japan
ina wanachama ambao ni wafanyakazi waliojiajiri pamoja na wanafunzi.