Atelekeza gari msituni likiwa na wahamiaji

0
586

Jeshi la Polisi mkoani Iringa kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji mkoani humo wamewakamata raia 16 wa Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila vibali.

Raia hao walikuwa wakisafirishwa na gari aina ya Landcruiser V8 linalodaiwa kuwa na namba usajili za Serikali.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema raia hao wa Ethiopia wamekamatwa katika maeneo ya msitu wa Luganga kata ya Sao Hilltarafa ya Ifwagi wilayani Mufindi wakiwa wametelekezwa kwenye shamba la mahindi.

Kwa mujibu wa Kamanda Bukumbi, dereva wa gari hilo lenye namba za usajili STL 3999 zinazodaiwa kuwa ni bandia alilitelekeza porini na kufunga milango na kutokomea kusikojulikana huku akiwaacha wahamiaji hao porini.

Uchunguzi wa awali umegundua kuwa gari hilo lilolokutwa na namba za Serikali limesajiliwa kwa namba T 803 CWV lenye chasis namba URJ 202-5001217 na linamilikiwa na Said Hassan mkazi wa Tabata mkoani Dar es Salaam.

Jeshi la polisi linaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo na mmiliki wa gari ambalo limetumika kusafirisha wahamiaji hao raia wa Ethiopia.