Uchaguzi mkuu waahirishwa Ethiopia

0
386

Uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini Ethiopia umeahirishwa hadi mwezi Juni mwaka 2021 kutokana na janga la virusi vya corona (Covid-19) linaloendelea kuikabili nchi hiyo.

Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya ndani vya nchi hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Ethiopia (NEBE) imefikia uamuzi huo baada ya kushauriana na vyama mbalimbali vya siasa.

NEBE imesema kuwa, uchaguzi mkuu nchini Ethiopia sasa utafanyika Juni 5 mwaka 2021 na kwamba tarehe hiyo pia inaweza kubadilika kulingana na hali itakavyokuwa.

Baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani nchini Ethiopia vimeitaka Serikali kugawana madaraka endapo uchaguzi mkuu hautofanyika.

Ethiopia ina muundo wa mabunge mawili, ambapo katika Bunge Kuu la Serikali kuna viti 112 na katika Baraza la Wawakilishi la Wananchi kuna viti 547.