Muhimbili yapanua huduma kwa wanachama wa NHIF

0
303

Kufuatia baadhi ya hospitali kusitisha huduma kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuanzia Machi 1, 2024, uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umekuja na mpango wa dharura wa kutoa huduma kwa wanachama hao ili waweze kuwa na mwendelezo wa huduma za kiafya.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo ya taifa imefanikiwa kuhamia kwenye kitita kipya cha mafao cha mwaka 2023 kilichopendekezwa na NHIF ambapo huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

Prof. Janabi amesema, Muhimbili imeongeza muda wa kuona wagonjwa katika kliniki zote za Upanga kupitia vyumba 75 vya kuona wagonjwa na vyumba vingine 59 vya kuona wagonjwa viliyopo Mloganzila kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nne usiku au mpaka mgonjwa wa mwisho atakapomaliza kuonwa na daktari.

“Tunajua kuna wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji (electives). Tunavyo vyumba 18 vya upasuaji Upanga na Mloganzila vyumba vya upasuaji ni 13. Kwa wagonjwa wenye tatizo la figo wanaohitaji kusafishwa damu, Upanga tunazo mashine 47 za kutoa huduma hiyo na tumeongeza zamu za kutoa huduma hiyo katika mzunguko wa saa nne wa kila zamu, kutoka tatu hadi nne kwa Upanga na Mloganzila ambapo kuna mashine 12 tumeongezea mizunguko kutoka miwili hadi minne na muda unaobaki ni wa kufanya matengezo kinga pamoja na usafi wa mashine hizo,” ameeleza Prof. Janabi.

Prof. Janabi amesema MNH kama mmoja wa watoa huduma wakubwa nchini nayo itaendelea kufuatilia utendaji wa kitita hicho ili kubaini changamoto zitakazojitokeza na kuziwasilisha kwa mamlaka husika.