Hivyo virutubisho kwenye mchele viwekwe hapa huku tunaona – Bashe

0
582

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametolea ufafanuzi juu ya mjadala ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu msaada wa chakula kwa wanafunzi wa Tanzania kutoka Marekani.

Bashe amesema kuwa ipo asasi isiyo ya kiserikali (NGO) inayofanya miradi katika shule za msingi na sekondari nchini ambayo ndio iliyopanga kuleta msaada huo wa chakula Tanzania kutokea nchini Marekani unaoaminika kuwekewa virutubisho.

Hata hivyo, amesema Wizara imeitaka NGO hiyo kuwajulisha Wamarekani kuwa Tanzania upo mchele wa kutosha na maharage, hivyo fedha ambazo nchi hiyo inazitumia kuwapa wakulima wa Marekani izitumie kununua chakula kwa wakulima wa Tanzania.

Waziri ameongeza kuwa ameshatoa maelekezo na kusisitiza kuwa virutubisho ambavyo vinatakiwa kuwekwa kwenye chakula hicho cha msaada ili kuzipa shule viwekwe hapa hapa nchini katika utaratibu ambao utashuhudiwa na Watanzania.

“Sasa tumewaambia kuwa mchele upo na maharage yapo kwenye nchi hii, kwa hiyo zile fedha wanazotumia kuwapa wakulima wa Marekani wawape wakulima wa Tanzania. Tununue huo mchele na maharage kutoka kwa wakulima wa Tanzania na virutubisho wanavyotaka kuweka tuweke hapa hapa Tanzania wote tunaona,” amesisitiza Bashe alipokuwa akizungumza katika hafla ya miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya Milimani City Jijini Dar es Salaam.