Watatu mbaroni kwa tuhuma za kuua kichanga kwa moto

0
291

Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, kwa madai ya kuhusika na tukio la kuchoma moto nyumba na kusababisha kifo cha mtoto mmoja wa miezi 11 katika kijiji cha Ngumbaru wilayani Siha mkoani humo.

Akizungumza wakati alipofika kujionea uharibifu uliotokea, Kamanda wa Polisi mkoani humo Simon Maigwa, amesema katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa akiwemo mama na bibi wa mtoto huyo.

Amesema tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku ambapo baada ya kushtuka moto ulikuwa umeshaunguza godoro ambapo hali ya mtoto pamoja na mama haikuwa nzuri na hivyo kupelekwa hospotali ya wilaya ya Siha kwa matibabu.

“Wakiwa hospitali ya wilaya ya Siha hali ya mtoto na mama yake haikuwa nzuri hivyo walikimbizwa kupelekwa hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kcmc ambapo mtoto alifariki,”-Amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amemtaja mtoto aliyefariki kuwa ni Jovin Adam huku majeruhi ni Julietha Charles na Dafroza Charles.

Amesema chanzo cha tukio hilo ni kumwagwa kwa kimiminika cha mafuta ya petrol na watu wasio na nia njema na kuwasha moto.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambapo watuhumiwa watafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.

Sauda Shimbo-Kilimanjaro