Watanzania watakiwa kuwapongeza walioiwakilisha nchi Olimpiki

0
137

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul (Mb) amewataka Watanzania kutopuuzia jitihada zilizooneshwa na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Riadha waliokwenda kushindana katika mashindano ya Olimpiki 2020 nchini Japan na kufanikiwa kuingia katika nafasi ya kumi (10) bora kwenye mbio ndefu za kilomita 42 barabarani.

Pauline ameyasema hayo wakati akiipongeza timu iliyoshiriki katika mashindano ya Olimpiki na kuiaga timu inayokwenda kushiriki mashindano ya Paralimpiki nchini Japan, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Niombe Watanzania wasipuuze jitihada zilizofanywa na wachezaji wetu wa riadha katika mashindano ya Olimpiki, bali tunatakiwa kuwapongeza kwa kulipambania Taifa katika mashindano hayo makubwa duniani licha ya kuwa na mabadiliko ya hali ya hewa lakini walipambana na tukamaliza katika nafasi ya kumi bora kwa mwanariadha wetu Alphonce Simbu kushika nafasi ya saba. Tunatakiwa tujifunze kuthamini vya kwetu,” amesema Pauline.

Aidha, amesema wizara yenye dhamana ya michezo inayosimamiwa na Waziri Innocent Bashungwa imedhamiria kuendelea kuinua michezo nchini pamoja na kuipa nguvu michezo ya kipaumbele iendelee kufanya vizuri.

“Niseme tu kwamba viongozi wa vyama ambao hawawajibiki wajitathmini, serikali yetu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ipo makini na haitawafumbia macho viongozi wa michezo ambao hawawajibiki,” amesema Pauline.