Wasichana wanawezeshwa bila wavulana kuachwa nyuma

0
111

Mratibu wa Mpango wa Shule Salama kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hilda Mgomapayo amesema Mpango wa Shule Salama kupitia mradi wa SEQUIP umejikita katika kuwezesha wasichana kupata elimu ya sekondari na stadi za maisha bila ya kuwaacha nyuma wavulana. Amesema dhamira ya serikali ni kuzifikia shule zote za Tanzania bara ambapo kwa awamu ya kwanza mradi utaanza na shule 2,000.

Akizungumza kwenye semina ya kunoa walimu wanaoshughulika na utekelezaji wa mradi huo wa SEQUIP, Hilda amesema kuwa mpango huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2020/2021 utachukua miaka mitano kukamilika.

Amesema mradi unafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tamisemi kwa ufadhili wa Shirika la Fedha Duniani. Semina hiyo inayofanyikia mkoani Lindi imeibua walimu kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Amesema malengo ya Mpango wa Shule Salama yamejikita katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia wanafunzi wote ili kudhibiti wanafunzi kukatisha masomo, utoro na hali ya kutokuwa tayari kushiriki katika mchakato wa kujifunza.

Kuimarisha utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi ili kuondokana na njaa pamoja na kuimarisha utawala na uongozi wa shule kwa ajili ya utekelezaji bora wa Mpango wa Shule Salama ni jukumu lingine la SEQUIP.

Aidha. Hilda amebainisha mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia ili kufikia malengo hayo kuwa ni kuimarisha huduma za ushauri na unasihi ambapo kila shule inatakiwa kuwa na walimu wenye weledi wa ushauri na unasihi, kuimarisha mfumo wa kushugulikia malalamiko na kuimarisha mawasiliano kati ya shule na jamii katika masuala yanayohusu unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ndani na nje ya shule.

Mengine ni kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa watoto walio katika hatari ya kuacha shule pamoja na kuwajengea walimu uelewa kuhusu uzingatiaji wa miiko na maadili ya ualimu, njia chanya za kinidhamu na mahusiano ya wanafunzi na walimu shuleni huku viongozi wa shule wakiimarisha uwazi na uwajibikaji pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.