Wanawake waongoza kwa maambukizi ya Ukimwi – Utafiti

0
686

Utafiti wa athari za Virusi vya Ukimwi kwa mwaka (Tanzania HIV Impact Survey 2022-2023), umeonesha kwamba Tanzania inarekodi maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi takribani 60,000 kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi.

Utafiti huo umeonesha pia kuwa zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanaishi na Virusi vya Ukimwi.

Kwa wastani, maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi kwa wenye umri wa miaka 15 ni makubwa zaidi kwa wanawake (5.6%) kuliko wanaume (3%) nchini Tanzania.

Hata hivyo, hali hii inaweza kuchangiwa na mwamko mdogo wa wanaume kupima maambukizi. Novemba 2023 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alisema takwimu zinaonesha wanaume hawajitokezi kupima na pia hawajitokezi kuanza kupata dawa, hivyo kusumbuliwa sana na magonjwa nyemelezi yanayotokana na virusi vya Ukimwi.

Kwa upande wa mikoa, utafiti umeonesha Njombe ikiongoza kwa kuwa na maambukizi zaidi, huku Kaskazini Pemba ikiwa na kiwango kidogo zaidi cha maambukizi (0.2%).