Mshindi wa Nobel mgeni rasmi tuzo za uandishi bunifu

0
196

Mshindi wa Tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 katika fasihi, Prof. Abdulrazak Gurnah, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itayofanyika Aprili 13, 2024 katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

Prof Gurnah ambaye ni Mtanzania anayeishi Uingereza atawasili nchini kwa mwaliko wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inayoratibu utoaji wa Tuzo hiyo, Dkt. Aneth Komba, amesema kuwa Profesa Gurnah atapokelewa na viongozi mbalimbali katika Kiwanja cha Ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere kesho Aprili 12, 2024 akitokea nchini Uingereza.

“Moja ya malengo ya tuzo hii ni kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika kazi kubwa aliyoifanya kwenye eneo la uandishi,” amesema Dkt. Komba.

Ameongeza kuwa kabla ya hafla ya tuzo hiyo, Prof. Gurnah atapata nafasi ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na waandishi bunifu nchini kwa lengo la kubadilishana nao mawazo mbalimbali kuhusu uandishi bunifu.

Pia amesema kwamba wageni wengine katika hafla hiyo ni waandishi maarufu kutoka nchi za Kenya na Uganda ambao wataungana na waandishi bunifu wa Tanzania katika hafla ya tuzo hiyo na watapata nafasi ya kutoa uzoeafu wao katika eneo la uandishi bunifu.

Prof. Gurnah, mwandishi mkongwe wa fasihi alikuwa mshindi katika tuzo ya Nobel ya mwaka 2021 iliyofanyika nchini Sweden.

Tuzo ya Taifa inajumuisha vipengele vya riwaya, ushairi na hadithi za watoto ambapo washindi wa kwanza katika vipingele hivyo watapata zawadi ya shilingi milioni kumi kila mmoja.

Tuzo hiyo inafanyika nchini kwa mara ya pili sasa ambapo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 2023 .