Kwa nini wanaoathirika zaidi na picha za utupu ni wanawake?

0
296

Tunaishi kwenye ulimwengu wa kidigitali, ulimwengu huu hutufanya sote kwa wakati fulani kuwa katika mstari wa kuwa wahanga wa matukio ya picha au video zetu kusambaa mitandaoni bila ridhaa yetu ikiwa tu hatutakuwa makini. Hebu fikiria, utakuwa katika hali gani pale utakapokutana na picha yako ya faragha mitandaoni?

Neno ‘connection’ limepata umaarufu katika siku za hivi karibuni hasa kila mara inapotokea picha au video za uchi zimesambaa mitandaoni.

Mara nyingi ‘connection’ inapovuja, wanaojitokeza kwenye kadamnasi kuomba msamaha ni wanawake, hata kama video hiyo inamuhusisha mwanamke na mwanaume, Je! Kwanini wanawake pekee?

Mtaalamu wa Saikolojia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Chriss Mauki amesema mwanamke huathirika kutokana na tamaduni iliyopo enzi na enzi.

“Hata yule mwanamke aliyepelekwa mbele ya Yesu kwa kosa la uzinzi alipelekwa mwenyewe bila mwanaume lakini lazima awepo mwanaume katika hilo, ndivyo jinsi utamaduni ulivyojengeka kwa mwanamke enzi na enzi”-amesema Dkt. Chriss Mauki.

Amesema kuongezeka kwa matukio ya uvujishaji wa picha za utupu ni kutokana na mmonyoko wa maadili, watu hawajali tena kulinda faragha zao.

Kuhusu namna ya kujinasua kutoka kwenye wimbi hili, Dkt. Chriss Mauki amesema wanawake wanapaswa kujilinda wenyewe hasa wanapokuwa faragha na wenzi wao kwa kuhakikisha analinda usiri wake.

“Kuepuka athari zaidi, kwanza mwanamke lazima ahakikishe analinda faragha yake, ajue aina ya mtu aliyenaye kwenye mahusiano na tabia yake, hii itapunguza kwa kiasi kikubwa.”

Kumbuka
Kutuma picha za faragha inaweza kuwa jambo la kufurahisha hadi pale utakapogundua kuwa maisha yako ya baadaye yameharibiwa! Hivyo, kabla ya kutuma hiyo picha au video kwa mwenza wako, kumbuka madhara ya muda mrefu yanayoweza kutokana na kitendo hicho.