Isome hapa hotuba ya Waziri Mkuu ya kuahirisha mkutano wa 18 wa Bunge

0
440
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 jijini Dodoma.

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA NANE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 7 FEBRUARI, 2020
UTANGULIZI

Shukrani
 Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa katika Mkutano huu wa Kumi na Nane wa Bunge lako Tukufu tukiwa buheri wa afya. Aidha, kwa kuwa huu ni Mkutano wa kwanza tangu mwaka huu uanze, ninakutakia wewe Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wenzangu, watumishi wa Bunge na Watanzania wote  Heri ya Mwaka Mpya 2020.

Salamu za Pole

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu za pole kwa Wananchi wa Jimbo la Newala Vijijini, kwako, kwa Bunge lako Tukufu na kwa familia ya Mbunge Rashid Ajali Akbar, aliyefariki tarehe 15 Januari, 2020.

 Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia za watu waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kwa familia za watu 20 waliofariki tarehe 01 Februari 2020 katika Ibada, mjini Moshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matukio hayo, Watanzania wamepokea kwa mshtuko taarifa kuhusu vifo vya wanajeshi wetu 10 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania vilivyotokea tarehe 03 Februari 2020 wakati wakishiriki mazoezi ya Kijeshi huko Msata, mkoani Pwani na Askari watatu wa Jeshi la Polisi waliofariki kwa ajali, mkoani Njombe. Natumia fursa hii kutoa pole kwa Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Inspekta Jenerali Simon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi na kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa askari hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wenzangu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kusababishiwa madhara mbalimbali kutokana na ajali za barabarani na matukio mengine. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema peponi na awape nafuu majeruhi wapone haraka.

Pongezi

 Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika mkutano huu wa Kumi na Nane wa Bunge lako tukufu, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walionitangulia kumpongeza Mhe. George Boniface Simbachawene (Mbunge wa Kibakwe) kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mbunge wa Ilala) kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira.

 Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Mabalozi wote ambao wamepangiwa vituo vya uwakilishi hivi karibuni. Natumia nafasi hii kuwakumbusha tena kuwa pamoja na mambo mengine, tutaendelea kupima utendaji kazi wao kwa namna wanavyovutia uwekezaji, kutangaza utalii, kutafuta masoko ya bidhaa zetu sambamba na kujenga taswira nzuri ya Tanzania katika maeneo yao ya uwakilishi.

Aidha, Viongozi wote mlioteuliwa, tambueni kuwa mnalo jukumu kubwa la kuwahudumia Watanzania hususan katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Spika, wewe Mheshimiwa Naibu Spika na watendaji wa Bunge kwa ubunifu na uthubutu ambao umekuwa chachu ya mageuzi makubwa ya kiutendaji katika Bunge hili. Katika hili, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipopongeza Bunge hili tukufu kwa kukabidhi majoho kwa Maspika Wastaafu ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao kwa Bunge hili na Taifa kwa ujumla. Hongera sana kwa Mheshimiwa Spika!

SHUGHULI ZA BUNGE

Maswali na Majibu

 Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkutano huu wa 18 tunaouhitimisha leo, jumla ya maswali 118 ya msingi na mengine 320 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na Serikali. Kadhalika, maswali 14 ya msingi na swali moja la nyongeza ya papo kwa papo yaliulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu.

Miswada ya Serikali

 Mheshimiwa Naibu Spika, katika mkutano huu, Bunge lako tukufu lilipitisha kwa hatua zake zote Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 8) wa mwaka 2019 na Muswada wa Sheria ya Usuluhishi wa mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, miswada ifuatayo nayo ilisomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge lako tukufu:

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2020;
Muswada wa Sheria ya Afya ya Mimea wa Mwaka 2020; na
Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu wa Mwaka 2020.

Maazimio ya Serikali

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliwasilisha katika Mkutano huu Azimio la kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyumba ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa Kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019.

Kamati za Kudumu za Bunge
 Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mkutano huu, Kamati za Kudumu za Bunge 15 ziliwasilisha Bungeni taarifa za mwaka za kazi. Taarifa hizo zilisheheni uchambuzi wa kina, maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa Serikali.

Nitumie fursa hii kuwapongeza Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wote wa kamati hizo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuanzia maandalizi ya kazi za kamati hadi kuwasilisha taarifa zao katika Bunge lako tukufu.

 Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea hoja zilizoibuliwa wakati wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge ambazo inaamini kuwa zimeibuliwa kwa malengo mazuri ya kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi na uwajibikaji. Serikali inaahidi kuzifanyia kazi hoja hizo hususan wakati huu tunapoelekea kwenye maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2020/2021.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2019/2020 KATIKA NUSU YA KWANZA YA MWAKA 2019/2020 (JULAI  – DESEMBA 2019)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama itakavyokumbukwa mwezi Juni, 2019 Bunge lako tukufu lilipitisha Mpango na Bajeti ya Serikali wa shilingi trilioni 33.1.  Kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida yalikuwa ni shilingi trilioni 20.85 na matumizi ya maendeleo yalikuwa shilingi trilioni 12.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Novemba, 2019 Serikali iliwasilisha katika Bunge lako Tukufu Muhtasari wa mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2019/2020 na mwelekeo kwa mwaka 2020/2021.

Kwa msingi huo, nimeona ni vema kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi baadhi ya mambo makubwa na mafanikio yaliyopatikana hadi kufikia mwishoni mwa Desemba, 2019 ambapo ni nusu ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi mahiri wa Jemadari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimedhihirika wazi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Viashiria vingi vya kiuchumi vinaonesha matokeo mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2019, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 6.8. Aidha, ukuaji wa uchumi kwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika robo ya tatu ya mwaka 2019 ulikuwa kama ifuatavyo: Kenya (asilimia 5.1); Uganda (asilimia 2.7); na Rwanda (asilimia 11.9).

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine juhudi za Serikali katika kuimarisha uwekezaji kwenye miundombinu ya msingi ya barabara, reli, na viwanja vya ndege; kutengemaa kwa upatikanaji wa huduma za maji; kuimarika kwa huduma za usafirishaji; habari na mawasiliano; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kumekuwa chachu ya mafanikio hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukuaji huo wa uchumi umechangia kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta rasmi na isiyo rasmi na hivyo, kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, mapato ya kodi yaliongezeka hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.52 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa shilingi trilioni 1.30 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na  kurahisisha ulipaji wa kodi, mapato ya kodi kwa mwezi Desemba, 2019 yaliweza kuvunja rekodi na kufikia shilingi trilioni 1.92.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa matumizi, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, Serikali imetumia shilingi trilioni 15.32, sawa na asilimia 91.2 ya lengo. Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ulipaji wa mishahara ya watumishi, ugharamiaji wa deni la Serikali, ulipaji wa madai ya ndani yaliyohakikiwa (watumishi, wazabuni na wakandarasi) na uendeshaji wa shughuli za Serikali katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuimarika huko kwa mapato kumewezesha Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi kupitia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii. Naomba japo kwa uchache Mheshimiwa Naibu Spika, nitaje mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019 ikiwa ni miezi sita ya mwaka wa fedha kama ifuatavyo:

Kuendelea kwa ujenzi wa reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge) kwa sehemu ya Dar es Salaam – Morogoro (KM 300) ambayo hadi Desemba 2019 ilifikia asilimia 70. Aidha, kazi za ujenzi kwa sehemu ya Morogoro – Makutupora (KM 422) zinaendelea vizuri na Serikali imerejesha huduma ya reli ya abiria na mizigo ya Kaskazini (Dar es Salaam – Moshi) na jitihada zinafanywa ili iweze kufika mkoani Arusha;

Kuendelea na ujenzi wa Mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambapo kazi zilizokamilika ni pamoja na: ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini wenye urefu wa mita 147.6 na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja;

Kuendelea na mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA) ambapo hadi Desemba 2019 jumla ya vijiji 8,236 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa na umeme, sawa na asilimia 67.1.

Aidha, kufuatia malalamiko ya ucheleweshaji wa baadhi ya miradi ya REA, namuagiza Waziri wa Nishati ahakikishe wakandarasi wote waliosambazwa kwenye mpango wa REA wanakamilisha majukumu yao kwa wakati;

Kuendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya 11. Hadi Desemba 2019, ndege nane zimepokelewa na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu yamefanyika. Aidha, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa marubani, wahandisi na wahudumu pamoja na kulipa madeni;

Kuzinduliwa kwa Jengo la Tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kuanza kutumika kuhudumia abiria; kuendelea na uboreshaji wa kiwanja cha ndege Mwanza na viwanja vya mikoa mbalimbali;

Kuendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya. Mtandao wa barabara kuu umefikia kilomita 8,502 na mtandao wa barabara za mikoa kilomita 1,756. Pia, Serikali imeendelea na ujenzi wa Ubungo inter-change ambapo hadi Desemba 2019 ulifikia asilimia 62 na ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha (asilimia 63);

Kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya: Sibiti (Singida), Momba (mpakani mwa Songwe na Rukwa), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Lukuledi (Lindi) na kuendelea na ujenzi wa daraja la Selander na daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa mita 3,200 na upana wa mita 28.45;

Kuboresha elimu ya msingi kwa kuendelea kutekeleza programu ya elimumsingi bila ada ambapo Serikali inagharamia chakula kwa wanafunzi 189,226 wa kutwa na bweni, posho ya madaraka kwa walimu wakuu 23,843, fidia ya ada kwa wanafunzi 1,874,331 na ruzuku ya uendeshaji wa shule.

Katika kipindi cha  Julai hadi Desemba 2019, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 128.1 kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada;

Kuimarisha elimu ya juu, ufundi na ustawi wa jamii kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambapo hadi Desemba 2019 jumla ya shilingi bilioni 266.4 zimetolewa kwa wanafunzi 130,072. Kati yao wanafunzi 49,493 ni wa mwaka wa kwanza na 80,579 wanaoendelea. Aidha, Serikali imeendelea kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike; kukarabati majengo ya vyuo vikuu na vyuo vya ualimu; kuboresha vyuo vya VETA kwa kujenga na kuboresha majengo ya vyuo na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Vilevile, Serikali imeimarisha vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kwa kuanzisha vituo vitano vya ubunifu sanjari na kutekeleza programu ya uanagenzi ili kupata ujuzi wa kujiajiri unaoendana na ushindani wa soko la ajira;

Kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kugharamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo 487 vya kutolea huduma za afya ikijumuisha vituo vya afya 320, hospitali za halmashauri za wilaya 70, hospitali za zamani tisa na zahanati 88. Aidha, Serikali imejenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Seko Toure, Burigi – Chato, Mwananyamala, na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali ya Kibong’oto na ujenzi wa Isolation centre katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Pia, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 320 za watumishi wa sekta ya afya pamoja na kugharamia ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo shilingi bilioni 334 zimetumika. Vilevile, katika kipindi hicho, jumla ya madaktari bingwa 311 wameendelea kulipiwa gharama za masomo ya uzamili katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Kadhalika, katika kipindi cha nusu ya pili, Serikali inakusudia kuajiri zaidi ya watumishi 4,000 wa sekta ya afya;

Kuendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama vijijini na mijini ambapo utekelezaji wa miradi 631 unaendelea ikijumuisha miradi 558 ya maji vijijini na 73 ya maji mijini. Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Arusha, mradi wa maji  wa Same–Mwanga-Korogwe na mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019, jumla ya shilingi bilioni 325.9 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji; ikiwemo uchimbaji wa visima  vifupi, vya kati na virefu;

Kuimarisha juhudi za ujenzi wa viwanda kwa kuboresha Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO), ukarabati na upanuzi wa kiwanda cha ngozi na bidhaa za ngozi cha Karanga – Moshi na kuimarisha Shirika la Nyumbu ili kuongeza uzalishaji ikiwemo kuzalisha magari ya zimamoto. Aidha, kumekuwa na ongezeko la ajira na uzalishaji viwandani hususan katika viwanda vya saruji, marumaru, chuma, kusindika matunda na mazao ya chakula ikijumuisha ubanguaji wa korosho. Kwa mfano, jumla ya tani 4,254 za korosho zilibanguliwa kupitia viwanda 17 ambavyo vilizalisha ajira za moja kwa moja 4,066;

Kuendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 37; ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 46; ukarabati wa meli ya MV Victoria umefikia asilimia 65 na MV Butiama asilimia 60. Kuendelea na ujenzi wa kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia; kuendelea kukarabati vivuko vya MV Sengerema (asilimia 40); MV Kigamboni (asilimia 60), na MV Utete (asilimia 95). Hatua nyingine ni kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha Kigongo – Busisi;

Upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam unaendelea ambapo ujenzi wa gati Na.1, 2 na 3 na gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) umekamilika na kuwezesha meli ya kwanza yenye uwezo wa kubeba magari 6,000 kuhudumiwa katika gati hilo. Aidha, uboreshaji wa bandari za Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu unaendelea;

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi sambamba na kuratibu vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati na kielelezo. Kama nilivyotangulia kueleza, miradi hiyo inayohusisha sekta ya miundombinu wezeshi, nishati, maji, afya na elimu imekuwa chachu ya kuboresha maisha ya Watanzania kupitia ukuaji wa sekta rasmi na isiyo rasmi.

ELIMU

Matokeo ya Mitihani ya Kitaifa

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya maboresho makubwa na uwekezaji katika sekta ya elimu nchini. Uwekezaji huo ni pamoja na kutoa Elimumsingi Bila Ada, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule sambamba na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa elimu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo chanya ya maboresho hayo ni kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika upimaji wa kitaifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na mitihani ya kitaifa kidato cha nne kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2019. Aidha, shule za kata nazo zimeendelea kufanya vizuri na kuongeza matumaini kwa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne mwaka 2019 yamebainisha kuwa jumla ya wanafunzi 1,531,120 walifaulu ikilinganishwa na wanafunzi 1,213,132 waliofaulu mwaka 2018. Ufaulu huo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.21. Kwa upande wa kidato cha pili, wanafunzi 514,251 walifaulu upimaji wa kitaifa kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wanafunzi 452,273 waliofaulu upimaji huo mwaka 2018 sawa na ongezeko la asilimia 13.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 wanafunzi 340,914 kati ya wanafunzi 422,722 walifaulu mtihani wa Taifa wa kidato cha nne. Aidha, ubora wa ufaulu wa wanafunzi nao umeongezeka kwa Mwaka 2019. Kwa mfano, wanafunzi 135,301 sawa na asilimia 32.01 walipata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu.

Maboresho ya miundombinu ya elimu

Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu yamekuwa chachu ya kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu na wakati mwingine kuleta changamoto kwenye miundombinu ya elimu. Hata hivyo, Serikali imeendelea kukamilisha usajili wa shule mpya, kuongeza vyumba vya madarasa 1,218 na mabweni 14 ili wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka 2020 waweze kuanza masomo kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee tena kusisitiza kuhusu maelekezo niliyoyatoa Desemba, 2019 kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwamba wahakikishe miundombinu ya shule inakamilika kwa wakati na wanafunzi wote waliofaulu wanapata fursa ya kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza.

KILIMO

Hali ya Kilimo

Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa 2019/2020 mvua zimeendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali kwa kiwango cha kuridhisha. Hata hivyo, baadhi ya maeneo mvua zimenyesha kwa wingi na kuathiri ustawi wa mazao na shughuli za kilimo. Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa imeendelea kutoa taarifa za mwenendo wa mvua na kutumia taarifa hizo kuwashauri wakulima kuzalisha mazao kulingana na kiasi cha mvua katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, Serikali imejiandaa kukabiliana na tishio la Nzige wa Jangwani ambao tayari wamevamia nchi za jirani. Serikali inafuatilia kwa karibu na kubaini endapo kuna viashiria au uwepo wa nzige hao kwa ajili ya kuchukua hatua za kuwadhibiti kwa wakati endapo watajitokeza. Serikali imeendelea kujipanga vizuri katika kudhibiti tishio hilo la nzige wa jangwani pamoja na visumbufu vyote vya mazao vitakavyotokea katika msimu huu wa kilimo.

Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongeza uzalishaji na tija kwenye kilimo, Serikali imeendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo. Hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 upatikanaji wa mbegu za kilimo ulikuwa tani 71,155. Kati ya hizo, tani 58,509 zimezalishwa hapa nchini, tani 5,175 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 7,469 ni bakaa ya msimu wa  2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mbolea, makisio ya mahitaji kwa msimu wa 2019/2020 ni tani 586,604 ikilinganishwa na tani 514,138 mwaka 2018/2019. Upatikanaji wa mbolea hadi kufikia tarehe 30 Januari, 2020 umefikia tani 410,499 sawa na asilimia 70. Aidha, kwa kuwa mbolea hizo hutumika kulingana na hatua za ukuaji wa mazao, Serikali inaendelea kuhakikisha asilimia 30 iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, viuatilifu vimeendelea kusambazwa kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mazao nchini. Mathalan, hadi kufikia tarehe 30 Januari 2020, zipo jumla ya tani 2,258 za salfa ya unga na lita 160,271 za viuatilifu vya maji vya zao la korosho kwa ajili ya msimu wa 2020/2021. Katika zao la pamba, hadi kufikia tarehe 30 Januari 2020, ekapack 802,000 zimesambazwa kwa wakulima na ununuzi wa ekapack 8,200,000 za viuatilifu na vinyunyizi 20,000 unaendelea.

Masoko ya Mazao ya Kilimo

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada za Serikali za kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara zinakwenda sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo yanayozalishwa nchini. Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya masoko ikiwemo mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao umeonesha matokeo chanya na kuwapatia faida wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani bei ya mazao ya ufuta na kakao imeongezeka. Kwa mfano, bei ya ufuta imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 1,000 mwaka 2017/2018 hadi kufikia shilingi 3,500 kwa kilo katika mwaka 2019. Aidha, bei ya kakao imeongezeka kutoka shilingi 3,200 msimu wa 2018/2019 hadi shilingi 5,000 kwa kilo katika msimu wa 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto zilizopo katika masoko ikiwemo miundombinu hafifu, matumizi duni ya mfumo wa TEHAMA, utunzaji hafifu wa kumbukumbu na malipo kwa wakulima wasiokuwa na akaunti au wenye kutumia akaunti za benki za wakulima wenzao. Hivyo, nitoe wito kwa wakulima kufungua akaunti kwa wakati na kuacha kutumia akaunti za wakulima wenzao ili wasicheleweshewe malipo na kuepuka udanganyifu kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika.

Utoaji wa Huduma za Ugani

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha utoaji wa huduma za ugani nchini ili kuongeza tija katika kilimo. Hatua hizo ni pamoja na kuwahamisha maafisa ugani wote kutoka Makao Makuu ya Halmashauri kwenda kwenye ngazi ya Vijiji, Kata na Tarafa. Hadi kufikia Desemba, 2019 jumla ya maafisa ugani 753 kati ya 1,120 wamehamishwa kwenda katika ngazi hizo. Nitumie nafasi hii tena kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakamilisha kuwahamisha maafisa ugani wote ambao bado hawajahamishwa.

Kuimarisha Ushirika

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kufanyia kazi malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu mwenendo usioridhisha wa baadhi ya Vyama vya Ushirika pamoja na watendaji wake. Lengo la Serikali ni kujenga ushirika imara na wenye kumpatia tija mkulima.

Hivyo, kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha vyama vya ushirika ili viwe na tija kwa wakulima. Mikakati hiyo, inalenga kujenga mfumo thabiti wa usimamizi na uhamasishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ni kufanya mabadiliko ya kiutendaji, kuajiri maafisa ushirika wapya na kuhamisha maafisa kutoka Makao Makuu kwenda Ofisi za Mikoa na Halmashauri ili kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika.

MASUALA YA MSISITIZO

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo baadhi ya masuala ambayo ningependa kuyawekea msisitizo kupitia hotuba yangu hii. Masuala hayo ni hali ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zoezi la usajili wa laini za simu, uboreshaji wa daftari la uandikishaji wapiga kura na utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini

Mheshimiwa Naibu Spika, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini kuanzia Oktoba, 2019 hadi Februari, 2020 zimesababisha vifo kwa watu waishio maeneo ya mabondeni, uharibifu wa nyumba, miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli na madaraja. Jumla ya barabara 73 na madaraja katika Mikoa 18 ziliathirika. Aidha, reli za Tanga hadi Arusha na Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma kwa nyakati tofauti nazo zililazimika kufungwa kwa muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara na reli katika maeneo yaliyoathirika zinarejea haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ili kuwafahamisha wananchi mwenendo wa hali ya hewa na kutoa tahadhari kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii. Nitumie fursa hii kuwataka wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kuhama sehemu za mabondeni na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini. Nichukue fursa hii kuwahimiza wananchi wachukue tahadhari kwa kuhama kutoka mabondeni na kwenda maeneo yaliyo salama.

Zoezi la usajili wa laini za simu

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba tarehe 27 Desemba 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili laini zote za simu kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alisisitiza kuwa ameongeza muda wa usajili hadi tarehe 20 Januari, 2020 na kwamba baada ya muda huo kwisha TCRA na Mamlaka nyingine husika zisitishe huduma kwa laini za simu ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 02 Februari 2020 kulikuwa na jumla ya laini za simu milioni 43.9. Laini milioni 31.4 sawa na asilimia 71.6 zilikuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole. Zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni endelevu. Uzimaji wa laini za simu unaendelea. Kwa msingi huo, nitoe wito kwa wananchi kwamba mara baada ya kupata namba ama kitambulisho cha uraia, nenda kwa wakala wa mtandao wako ili usajili laini yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawahimiza wananchi wote ambao hawajasajili laini zao za simu kwa sababu mbalimbali na wale ambao wanaendelea na zoezi la kupata vitambulisho vya uraia na wamekwishapata namba za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wasajili laini zao za simu kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa NIDA wasogeze huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata namba za vitambulisho kwa ajili ya kuwawezesha kusajili laini zao za simu na vilevile, kupata Vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mengine muhimu.

Daftari la Uandikishaji Wapiga Kura

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya kwanza. Hadi kufikia tarehe 02 Februari, 2020 imekamilisha uandikishaji wa Wapiga Kura katika Kanda ndogo kumi na mbili kati ya kumi na nne zilizopangwa katika ratiba ya uboreshaji wa awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanda ndogo 12 zilizokamilika zinahusisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Simiyu, Mwanza, Geita, Shinyanga, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tabora, Singida, Dodoma, Songwe, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Njombe, Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro (Ulanga DC na Malinyi DC) na Tanzania Zanzibar. Aidha, kanda ndogo ya kumi na tatu inayohusisha Mkoa wa Morogoro zoezi la uboreshaji limeanza tarehe 3 Februari, 2020 na litakamilika tarehe 9 Februari, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, uandikishaji wa wapiga kura ni wa siku saba kwa kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Aidha, zoezi la uboreshaji linahusisha uandikishaji wa wapiga kura wapya ambao hawajahi kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, urekebishaji wa taarifa za wapiga kura walioandikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa ikiwemo waliofariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wapiga kura walioandikishwa kuanzia kanda ndogo ya kwanza hadi kanda ndogo ya 12 walikuwa 18,058,977. Jumla ya wapiga kura 2,012,212 wamejitokeza kuboresha taarifa zao sawa na asilimia 11.14 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wapiga kura wapya walioandikishwa katika Kanda ndogo zote 12 ni 5,666,343 ambayo ni sawa na asilimia 31.38 ya idadi ya Wapiga Kura walioandikishwa mwaka 2015 katika Kanda ndogo zote 12. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 14.38 la makadirio ya awali (asilimia 17).

Vilevile, idadi ya wapiga kura walioondolewa kwa kupoteza sifa ni 14,894 ambayo ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 katika kanda ndogo zote 12.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Tume kuongeza kasi ya uandikishaji. Kadhalika, natoa rai kwa wananchi kutumia haki yao hiyo ya kikatiba na kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kuboresha taarifa zao na kujiandikisha upya kwa wale wenye umri wa miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo Oktoba, 2020.

Migogoro ya Ardhi

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko la shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na hivyo, kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji na uwekezaji. Hali hiyo, imesababisha migogoro, malalamiko na kero mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi katika baadhi ya maeneo nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi nchini inatatuliwa kwa njia ya amani. Aidha, katika kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kibali kwa vijiji 920 kati ya 975 vilivyokuwemo ndani ya hifadhi na mapori na maeneo ya hifadhi kuhalalishwa rasmi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa, Serikali imeanza utekelezaji wa agizo la Mheshimwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi kwa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa 26 na kuimarisha ofisi za ardhi za halmashauri zote badala ya ofisi za ardhi za kanda.

MICHEZO

Mheshimiwa Naibu Spika, sanaa imeendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa na hata katika kutengeneza ajira. Kwa mfano, kwa mwaka 2018/2019 sekta hiyo ilichangia asilimia 0.29 katika ukuaji wa Pato la Taifa. Niwapongeze wasanii wetu kwa kuendelea kulitangaza vyema Taifa letu na fursa zake na hivyo, kuchangia maendeleo ya nchi yetu kupitia utalii na uwekezaji. Wasanii wa muziki wa bongo fleva, maigizo, uchongaji na uchoraji wamechomoza katika kuongeza Pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mpira wa miguu tunampongeza mchezaji wetu, Mbwana Samatta kwa kuweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Uingereza katika Klabu ya Aston Villa. Tunamtakia kila la kheri katika Ligi Kuu ya Uingereza ambayo ni moja ya ligi ngumu, maarufu na yenye ushindani mkubwa duniani. Nitoe rai kwa wachezaji wetu wa ndani, nao kujifunza kupitia mafanikio ya Samatta kwa kuongeza bidii, nidhamu na kiu ya mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nizipongeze timu zetu za wanawake za umri wa miaka chini ya 20 (U-20) na miaka 17 (U-17) kwa kuendelea kufanya vyema kuelekea kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2022. Wakati timu ya wanawake U-20 ikipata ushindi wa nyumbani na ugenini dhidi ya Uganda, timu ya wanawake U-17 nayo iliiondosha Burundi kwenye mashindano kwa jumla ya magoli 6-1. Naipongeza pia Kilimanjaro Queens kwa kuchukua ushindi wa pili wa CECAFA. Kwa mafanikio hayo ya soka nchini kwa wanawake, nalipongeza Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa usimamizi mzuri bila kumsahau Mlezi wa Timu za Wanawake, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza pia vijana wetu wa kiume chini ya miaka 20 ambao walifanikiwa kuwa mabingwa wa michuano ya mpira wa miguu kwa CECAFA nchini Uganda. Nampongeza sana kijana wetu Kelvin John kwa kusajiliwa na timu ya GENK ya Ubelgiji kwenye Kikosi chao cha U-20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ndondi nako tumeendelea kufanya vizuri. Nitumie nafasi hii kumpongeza bondia wetu Salim Mtango ambaye tarehe 31 Januari, 2020 alimtwanga Bondia Surriya Tatakhun kutoka Thailand kwa Technical Knock Out (TKO).

Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyofahamu, Timu yetu ya Bunge ilishiriki Michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki Kampala, Uganda kuanzia tarehe 8 hadi 18 Desemba, 2019. Katika Michezo hiyo timu yetu ya Bunge ilifanikiwa kupata jumla ya medali 18. Medali hizo zilihusisha dhahabu tano, fedha 10 na shaba tatu. Nitumie fursa hii kuipongeza timu ya Bunge kwa mafanikio hayo pamoja na kulitangaza vema Bunge letu huko nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii angalau kuwatambua kwa majina Waheshimiwa Wabunge waliotuletea medali za dhahabu kama ifuatavyo:

Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Anatropia Theonest;
Mhe. Esther Matiko;
Mhe. Yosepher Komba; na
Mhe. Rose Tweve.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutambua juhudi za Bwana Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo na fujo isiyoumiza katika kutangaza nchi yetu, vivutio vyetu vya utalii pamoja na lugha ya Kiswahili. Ameonesha uzalendo wa kuitangaza nchi yetu licha ya kuwa yeye si Mtanzania. Hivyo, natumia fursa hii kuwapongeza wanamichezo pamoja na wasanii ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu sambamba na kujipatia kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa kwa sasa michezo na sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira na kipato hususan kwa vijana. Aidha, nisisitize kuwa michezo ni kinga na tiba kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na unene uliopitiliza. Kutokana na faida hizo, niendelee kutoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika michezo. Aidha, Serikali kwa upande wake itaendelea kuweka mfumo bora wa kisera na kisheria ili kuhakikisha sekta ya michezo inakuwa na kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa.

HITIMISHO

Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mbalimbali muhimu katika kuboresha maisha ya wananchi wetu. Nimshukuru Katibu wa Bunge na wasaidizi wake kwa huduma nzuri na msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia kwa kipindi chote tulichokuwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia watendaji wa Serikali na taasisi mbalimbali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri na ufanisi mkubwa na hivyo, kufanikisha shughuli zilizopangwa na Bunge lako tukufu bila kuwasahau wanahabari kwa uchambuzi wa hoja na mwenendo mzima wa Bunge na kufikisha habari hizo kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma ambazo wamekuwa wakizitoa kwa washiriki wa Bunge hili. Pia, niwashukuru madereva wote waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa. Nawatakia heri katika safari ya kurejea nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 31 Machi, 2020 siku ya Jumanne saa tatu kamili asubuhi katika ukumbi huu jijini Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.