Hatua 3 za Samia kufuatia mafuriko

0
142

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matatu ambayo ni utekelezaji wa Serikali kutokana na changamoto ya mafuriko yaliyoikumba nchi katika maeneo mbalimbali.

Mosi ni kurejesha utulivu. Katika hili, Rais amesema, “Tutarejesha utulivu katika mikoa iliyoathirika (na mafuriko). Viongozi wote muwajibike ipasavyo kwenye maeneo yenu.”

Pili, Rais ameagiza viongozi kushirikiana na wananchi. Rais Samia amesema kuwa baadhi ya maeneo yaliyoathirika ni yale ambayo mafuriko yamekuwa yakujirudia mara kwa mara kwa kuwa kiasili ni maeneo yaliyo mabondeni au yako kwenye njia za asili za maji.

Katika hili amesema ni jukumu ya viongozi kupunguza madhara na kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mvua na mafuriko kwa kushirikiana na wananchi.

“Hatuwezi kuzuia mvua kubwa na mafuriko moja kwa moja lakini tunaweza kupunguza madhara na kuimarisha jitihada za kukabiliana na athari za mvua na mafuriko. Kwa hiyo niwatake viongozi wote katika maeneo yetu kushirikiana na wananchi kuhakikisha tunapunguza athari za mafuriko,” amesema Rais Samia

Agizo la tatu Rais amesema ni kufanyika kwa uchunguzi wa kina. “Serikali tutafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu halisi za mafuriko kwenye maeneo hayo ili tuweze kuchukua hatua zitakazoondoa tatizo hili kwa muda mrefu.”

Rais Samia ameyasema hayo wakati akishiriki kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine, Monduli, mkoani Arusha.