Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Bashiru Ally, ameahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na weledi mkubwa ili kuwahudumia wananchi ikiwa ni njia ya kumuenzi aliyekuwa katibu mkuu kiongozi Hayati Balozi John Kijazi.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Balozi Dkt. Bashiru amesema, kwa sasa majukumu yaliyo mbele yake ni kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa ahadi za Rais kwa wananchi.
Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa awali alikuwa akisimamia serikali itekeleze ahadi na Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 lakini kwa sasa anaanza jukumu la kutekeleza ilani hiyo iliyobeba matumaini ya wananchi.
Aidha Dkt. Bashiru ameahidi kuendelea kusimamia dhana ya mawasiliano baina ya serikali na wananchi ili kurahisisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya serikali yanayowahusu wananchi kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema, bunge litaendelea kushirikiana na katibu mkuu kiongozi ili utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu serikali na bunge yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amemuahidi ushirikiano mkubwa katibu mkuu kiongozi katika utekelezaji wa majukumu yake.