Boko Haram wakiri kuwateka nyara Wanafunzi 333

0
188

Wanamgambo wa Boko Haram wamekiri kuhusika na tukio la kuwateka nyara Wanafunzi wa kiume 333, katika shule moja ya sekondari ya bweni kwenye jimbo la Katsina nchini Nigeria.

Ujumbe wa sauti uliorekodiwa wa mtu aliyejitambulisha kama kiongozi wa Wanamgambo hao, – Abubakar Shekau umeeleza kuwa, wameamua kuwateka nyara Wanafunzi hao ikiwa ni moja ya njia za kupinga mfumo wa elimu wa nchi za Magharibi.

Uongozi wa jimbo la Katsina analotoka Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria umesema kuwa, kwa sasa wanafanya mazungumzo na  Wanamgambo hao wa Boko Haram ili Wanafunzi hao waweze kuachiwa huru.

Hivi karibuni, watu wenye silaha waliishambulia shule hiyo ya sekondari ya Wavulana inayomilikiwa na Serikali na kuwateka nyara Wanafunzi hao na miongoni mwao wana umri wa chini ya miaka 10.

Tangu mwaka 2009, Wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakifanya mashambulio ya mara kwa mara nchini Nigeria hasa katika eneo la Kaskazini Mashariki, mashambulio ambayo yamesababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili kuyakimbia makazi yao.