Bilioni 5 kumaliza tatizo la maji Kibamba

0
297

Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepanga kutumia shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaomaliza kabisa tatizo la maji katika baadhi ya maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya DAWASA na kwamba mradi huo utasaidia kumaliza tatizo la maji ambalo limekuwa likiwasumbua kwa kiasi kikubwa wakati wa Msakuzi, Majengo, Luguruni, Magari Saba, Kwa Gama, Makabe na maeneo mengine.

Waziri Aweso amesema hata kuwa na msamaha na mtu yoyote ambaye atashiriki kuhujumu mradi huo na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaohujumu mradi huo wa maji.

Awali akitoa taarifa za mradi huo Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Cyprian Luhemeja amesema, mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 na kwamba utasaidia kumaliza tatizo la maji kwenye vitongoji vingi vya wilaya ya Ubungo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kibamba, Mbunge wa Jimbo hilo Issa Mtemvu amesema, DAWASA wametekeleza kwa vitendo ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.