Bashungwa : Nileteeni majina tuwachukulie hatua

0
93

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kuwasilisha majina ya Mameneja wa Kanda na Mikoa wa TEMESA ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili waweze kuchukuliwa hatua.

Bashungwa ametoa agizo hilo jijini Dodoma kufuatia kupokea malalamiko mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA ikiwemo huduma ya Kivuko cha MV. Tanga mkoani Tanga ambapo amemuagiza Katibu Mkuu kuingilia kati kubaini changamoto zinazokwamisha kivuko hicho.

“Mambo mengi ya kiutendaji yanaletwa kwa Waziri na Katibu Mkuu wakati Watendaji mpo na tumewaamini kusimamia taasisi zenu, hasa jambo hili lipo TEMESA. Mtendaji Mkuu kama kuna mapungufu ya wasaidizi wako bora uje kwa Katibu Mkuu useme huyu hatufai aondoke kuliko kukaa nao maana hatimaye litakuangukia wewe,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Aisha Amour kuangalia namna bora ya usimamizi wa TEMESA katika huduma ya vivuko nchini ili kuleta manufaa na uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ziimarike.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala amekiri kuwepo kwa changamoto katika Kivuko cha MV. Tanga na kusema kuwa timu ya wataalam inaendelea na marekebisho ya kivuko hicho ili kuboresha huduma zake.