‘Super Tuesday’ yaimarisha uwezekano wa Trump, Biden kuchuana tena

0
139

Rais Joe Biden wa Marekani na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump wamepata ushindi mkubwa katika takribani majimbo yote yaliyokuwa yakiendesha kura za maoni kwa ajili ya uteuzi wa wagombea urais wa vyama vikubwa vya Demokrati na Republican siku ya jana, maarufu Super Tuesday.

Kulingana na uchambuzi wa Kampuni ya Utangazaji ya CBS, hatua hii inaimarisha uwezekano mkubwa wa miamba hiyo miwili, Joe Biden na Trump kuchuana tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Novemba 5 mwaka huu, kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.

Kadiri wagombea hao wanavyopata wajumbe wengi zaidi wa kuwaunga mkono, ndivyo kila mshindani anavyokaribia kupata kibali rasmi kutoka kwa chama chake ili kuwania urais katika uchaguzi huo ujao.

Pande zote mbili zimeshinda katika majimbo yenye wajumbe wengi kama California, Texas, Virginia na Carolina Kaskazini.

Kura za maoni zilionesha Trump akimwacha mbali mpinzani wake katika Republican, Balozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, huku baadhi ya wapiga kura wakisema masuala ya uhamiaji na uchumi ambayo ni silaha kubwa za Trump ndiyo yanayowavuta kutaka agombee tena urais.

Majimbo yanayofanya kura za maoni katika Super Tuesday huwa na wajumbe zaidi ya theluthi moja ya wajumbe wote katika mchakato mzima wa uteuzi.

Mkusanyiko huu mkubwa wa kura za maoni ulianza 1988, na tangu wakati huo mgombea wa Republican anayepita mchujo katika Super Tuesday ndiye pia hufanikiwa kuwania urais wa Marekani.