NEMC yapata suluhu ya vibali kwa wachimbaji wa mchanga

0
262

Wachimbaji wa mchanga kwakutumia machepe na wakandarasi wa Mkoa wa Dar es salaam wamesema kutolewa kwa mwongozo na vibali vya kutolea mchanga kwenye mito kutawapunguzia usumbufu wa kukamatwa na Jeshi la polisi katika kujitafutia mkate wao wa kila siku.

Wachimbaji hao wametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wao maalumu na watendaji wa NEMC ili kupitia utekelezaji wa muongozo wa vibali iliokuwa umetolewa na waziri mwenye dhamana.

Kauli ya wachimbaji hao imekuja ikiwa imepita mwezi mmoja tangu aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa rais Ummy Mwalimu kutoa mwongozo wa usafishaji wa mito na utoaji wa michanga kwenye mito Mkoa wa Dar es Salaam katika kuokoa mali na maisha ya watu katika maeneo yao wanayishi.

“Tunashukuru Serikali kupitia Waziri aliyekuwa na dhamana na Mazingira kwakutupigania wachimbaji hatimaye tumepata vibali vya kutoa mchanga kwenye mito kwani awali tulikuwa tukipata shida na askari polisi ikiwa ni pamoja nakupigwa faini kubwa” wameeleza wachimbaji hao.

Katika muongozo huo Watendaji wa NEMC, tume ya madini, wasimamizi wa mabonde, Tarura na Tanroad walipewa wajibu kusimamia zoezi la Utoaji wa vibali kwa wachimbaji hao wa mchanga na wakandarasi tofauti na ilivyokua awali ili kusaidia wananchi kupata huduma stahiki ikiwa ni pamoja nakuisaidia Serikali kupata Mapato yake kuwahudumia wananchi wake bila usumbufu.

Kwa Upande wake Meneja wa NEMC kanda ya Mashariki Kaskazini Anorld Mapinduzi amesema watendaji wa Serikali za Mtaa wanajukumu la kusimamia miongozo inatolewa na Baraza la uhifadhi na Usimamizi wa mazingira NEMC ili kulinda afya za wananchi na Mazingira yao wanayoishi.

Kuhusu magari ya mchanga yanayofanya kazi usiku amesema kuwa ni suala linalotakiwa kuchukuliwa hatua ya haraka na wahusika pia kutakiwa kuacha kufanya hivyo ili kuepusha hatari zinazoweza kuwapata wananchi.

Zaidi ya vikundi arobaini vinavyojihusisha na Utoaji wa mchanga kwenye mito na wakandarasi vimefanikiwa kupata vibali huku baadhi vikishindwa kupata vibali hivyo kutokana na kushindwa kukidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine Meneja huyo ameongeza kuwa suala la mifuko na vifungashio vya plastiki limeelezwa kuwa changamoto kubwa inayoathiri mazingira hivyo kuhitaji wazalishaji kuzingatia sheria zilizowekwa juu ya uzalishaji wa mifuko hiyo vilivyowekwa na TBS.

“Changamoto ya mifuko ya plastiki bado ni changamoto kubwa kwenye jamii na elimu inahitajika kwa kiasi kikubwa hivyo tunapaswa kujua hakuna anayependa kuona kizazi chake kinaangia kutokana na sumu ya plastiki” amesema Meneja huyo.

Ameongeza kuwa athari za mifuko ya plastiki lina athari kwa viumbe hai wote wakiwemo viumbe wa baharini na nchi kavu hivyo jamii nzima inahitaji kupata elimu mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yasiyotibika ikiwemo kansa.