Mtuhumiwa wa mauaji ya 1994 Rwanda akamatwa Marekani

0
442

Eric Tabaro Nshimiye, mzaliwa wa Rwanda amekamatwa huko Ohio, Marekani kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Waendesha mashtaka wa Shirikisho wanamtuhumu Nshimiye kwa kuficha uhusika wake kwenye mauaji ya halaiki, ikiwa ni pamoja na kuwanyonga watu kadhaa kwa mkono wake hadi kufa.

Nshimiye ameishi Ohio tangu 1995 baada ya kupata hadhi ya ukimbizi nchini Marekani kwa njia ya udanganyifu, waendesha mashtaka wanasema.

Alikimbia Rwanda katikati ya mwa 1994. Mwaka uliofuata alikwenda Kenya, ambako anatuhumiwa kuwadanganya maofisa uhamiaji wa Marekani kwa kutumia vielelezo bandia na kufanikiwa kuingia Marekani.

Anatarajiwa kufikishwa baadaye katika mahakama ya shirikisho huko Boston, nchini Marekani.

“Bw. Nshimiye anashutumiwa kwa kusema uwongo ili kuficha ushiriki wake katika mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu kuwahi kutokea,” Wakala Maalumu wa Uchunguzi wa Usalama wa Ndani, Michael Krol amesema katika taarifa.