Mtu mpweke zaidi duniani afariki dunia

0
969

Mtu wa mwisho aliyebaki kutoka kikundi kimoja cha asili nchini Brazil amefariki dunia, akikadiriwa kuwa na umri wa miaka 60.

Habari kutoka nchini Brazil zinaeleza kuwa, mtu huyo mwanaume ambaye jina lake halijawahi kufahamika, ameishi peke yake kwa takribani miaka 26 katika eneo la Tanaru.

Jina alilokuwa akijulikana zaidi ni ‘’Mtu mpweke zaidi duniani’’.

Mwili wa mwanaume huyo uligundulika tarehe 23 mwezi huu kwenye chandarua nje ya kibanda chake kilichojengwa kwa kutumia nyasi.

Polisi katika mji wa Tanaru wamesema kifo cha mtu huyo ni cha kawaida, kwa kuwa katika eneo alipokutwa amefariki dunia hakukuwa na dalili zozote za mapambano, lakini hata hivyo wanafanya uchunguzi zaidi.

Mtu huyo alikuwa wa mwisho kati ya kundi la wenyeji ambalo watu wengine sita wa jamii yake waliobaki waliuawa mwaka 1995 katika eneo hilo la Tanaru.

Watu wengi wa kabila la “Mtu huyo Mpweke zaidi duniani” waliuawa mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Kwa muda mrefu , ‘’Mtu huyo mpweke’’ alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na Shirika linaloshughulikia Masuala ya Wenyeji la Brazil, ambapo mwaka 2018 alirekodiwa alipokuwa anapambana na mnyama pori na tangu wakati huo hakujawahi kutolewa taarifa zozote zinazomuhusu.