Libya wakubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa

0
175

Viongozi wa serikali mbili zinazohasimiana nchini Libya wamekubaliana kuunda serikali moja ya umoja wa kitaifa, jambo linaloashiria maendeleo katika kumaliza mkwamo wa kisiasa ambao umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao wamesema wamekubaliana juu ya “umuhimu” wa kuunda serikali mpya ya umoja ambayo itasimamia uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu na “kuunganisha nyadhifa kuu”.

Mazungumzo hayo yalifanyika katika mji mkuu wa Misri, Cairo, na yaliongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit.

Mazungumzo yalihusisha Rais wa Baraza la Rais wa Libya na mkuu wa Baraza Kuu la Serikali, wote wakiwa na makao yao jijini Tripoli, pamoja na spika wa Baraza la Wawakilishi katika utawala hasimu wenye makao yake makuu mjini Benghazi.

Libya ilianza kuvunjika vipandevipande baada ya kuangushwa kwa utawala wa muda mrefu wa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Nchi hiyo imegawanyika kati ya serikali inayotambulika kimataifa upande wa magharibi, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa mpito Abdul Hamid Dbeibah mjini Tripoli, na utawala wa mashariki unaoungwa mkono na mwanajeshi Khalifa Haftar mjini Benghazi.