Wawekezaji kutoka India kutembelea Tanzania

0
3498

Wawekezaji mbalimbali kutoka nchini India wanatarajia kuja kuwekeza nchini Tanzania ambapo kundi la kwanza la wawekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa viwanda vya madawa ya binadamu na vifaa tiba kutoka India, linatarajiwa kutembelea Tanzania kuanzia tarehe 19 Aprili 2022 ili kukutana na wadau na kuanza taratibu za kuwekeza Tanzania.

Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Mbega ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi hiyo kuendelea kuja kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali za uwekezaji.  

Balozi Mbega ametoa wito huo baada ya kufanyika kwa kongamano kubwa la biashara na uwekezaji (Tanzania India Trade Conference) lililofanyika katika jiji la Chennai, nchini India

Aidha Balozi Mbega ameongeza kuwa licha ya India kuwekeza nchini mtaji wa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 3.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa ya tano kwa uwekezaji, lakini bado nchi hiyo ina fursa kubwa ya kuongeza uwekezaji wake nchini

Wafanyabiashara wengine walioshiriki Kongamano hilo wameonesha nia ya kushiriki maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yataanza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022, Ushiriki huo utawawezesha kukutana na wafanyabiashara na kuona bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania.

Kupitia kongamano hilo, wazalishaji wa bidhaa za Ngozi na korosho wa Tanzania wameunganishwa na wafanyabiashara wa India ambapo watapata fursa ya kuuza bidhaa hizo katika soko la India

Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini India na Taasisi ya Uchumi na Biashara ya India (Indian Economic Trade Organization) limetoa fursa kwa taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara ikiwepo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania