Zanzibar yaanza kutoa vitalu uchimbaji mafuta, gesi

0
244

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amewahakikishia wawekezaji wote wa sekta ya mafuta na gesi mazingira mazuri ya uwekezaji kwa manufaa ya wote.

Dkt.Mwinyi amesema hayo alipokuwa akizindua duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu kwa kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia maeneo ya baharini Zanzibar.

Amesema dhamira ya Serikali katika uchumi wa Buluu ni kuimarisha uchumi wa nchi kwa haraka na kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu ya vyanzo vya nishati ya uhakika.

Kwa mujibu wa Rais Mwinyi, Serikali inaamini kuwa uchumi wa Buluu una fursa nyingi za kukuza mipango ya maendeleo ya kiuchumi yenye lengo la kupunguza umasikini na kutengeneza fursa za ajira.