Wanakijiji Waililia Serikali kuboresha miundombinu Shule shikizi ya Mtakuja

0
235

Wakazi wa kijiji cha Luhindo Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, wameiomba Serikali kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa jengo la Vyumba vitatu vya Madarasa ya Shule ya msingi shikizi ya Mtakuja walioianzisha ili kupunguza adha ya Watoto wao kufa kwa ajali pindi wanapovuka barabara kuelekea Shule Mama ya Msingi ya Wami Luhindo.

Wakizungumza na Kipindi cha Mirindimo ya TBC Taifa leo Aprili 8, 2022, wanakijiji hao wamesema Shule hiyo shikizi imesaidia Watoto wao kuwa na ari ya kusoma kwa bidii kutokana na Jengo la kisasa la Vyumba vitatu vya Madarasa lililojengwa kwa fedha za Uviko 19.

Licha ya mafanikio hayo, wanakijiji hao pamoja na Walimu wametaja changamoto nyingine zinazowakabili ni pamoja na miundombinu ya Barabara, Maji, viwanja vya michezo, Ofisi za Walimu pamoja na Vyoo.

Wanakijiji hao wameeleza kuwa, kupitia michango mbalimbali na kujitolea wamefanikiwa kujenga Jengo la Vyumba vya Madarasa vitatu ili kuongeza Madarasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuingia Darasa la tatu mwakani, hivyo wameiomba Serikali kuwasaidia kukamilisha ujenzi wa jengo hilo mapema iwezekanavyo.