Wadau waendelea kutoa misaada Katesh

0
185

Misaada mbalimbali imezidi kutolewa kwa waathirika wa janga la maporomoko ya tope na mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara na kusababisha vifo vya watu, majeruhi na uharibifu wa mali.

Katika kuunga mkono kuwafariji wananchi hao, Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imetoa pole kwa wananchi walioathirika kwa kutoa mitungi ya gesi 200 yenye ujazo wa kilo 15 kuwsaidia katika kipindi hiki kigumu.

Mitungi hiyo ya gesi ikiwa na majiko yake, imetolewa imekabidhiwa kwa Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendiga.

Akizungumza wakati wa kupokea mitungi hiyo Waziri Mhagama ameishukuru kampuni ya Oryx kwa mchango wake kwa wananchi wa Hanang kwani umekuja wakati muafaka kusaidia wananchi hao kwa kuwapatia nishati safi ya kupikia katika wakati huu mgumu.

Mkuu wa Idara ya Mauzo wa Kampuni ya Oryx Gas, Shaban Fundi amesema kampuni hiyo imefika Hanang katesh kuungana na kuwapa pole watanzania wenzao waliofikwa na janga la mafuriko na maporomoko.

“Tunajua kwa hakika wenzetu wameathirika sana katika kipindi hiki ni gharama kubwa kupata vyanzo vya moto kupikia. Oryx Gas tumekuja kukabidhi majiko 200 na mitungi ya gas ujazo wa kilo 15 kwa waathirika wa tukio hili, ” amesema Fundi.