Anayejifungua mtoto njiti kuongezewa siku za mapumziko

0
217

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), kimesaini mkataba wa hali bora na watumishi wake unaolenga kuboresha maslahi yao katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Hery Mkunda amesema kuwa kwa mara ya kwanza mkataba umeongeza idadi ya siku za mapumziko kwa mfanyakazi mwanamke atakayejifungua mtoto njiti na kufanya TUGHE kuwa Chama cha kwanza kuweka kipengele hicho katika mkataba wake wa hali Bora.

Mkunda amesema kuwa lengo la kuboresha kipengele hicho ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na Wanawake ndani ya TUGHE na kwa kufanya hivyo kutaongeza tija na ufanisi ndani ya chama.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo Makamu Mwnyekiti wa TUGHE Taifa, Dkt. Jane Madete ameeleza kuwa amefurahishwa na uamuzi huo wa kufikia makubaliano hayo kati ya Uongozi na wafanyakazi kwani utaenda kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii na kukifanya Chama kipige hatua mbele zaidi.