Viongozi wa kisiasa wapewa somo

0
2619

Viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya Taifa na kuepuka kuanzisha vyama kwa maslahi binafsi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Mohammed Ally Ahmed wakati wa kufunga mafunzo kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili  kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao wa namna ya kuendesha vyama vyao kama taasisi.

“Linapotokea zuri basi tuseme hili ni zuri na linapotokea baya tuseme hili lina tatizo kwa maslahi mapana ya taifa letu, utitiri wa vyama vya siasa pekee hautasaidia taifa kama vyama hivyo havitakuwa na nguvu ya kufanya kazi ama kuonyesha uzalendo wa kuendesha taifa”, amesisitiza Ahmed.

Naibu Msajili huyo wa vyama vya siasa nchini ametoa wito kwa viongozi hao wa kitaifa wa vyama vya siasa kuunga mkono jitihada za serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa za kuvijengea uwezo vyama hivyo  na kuongeza kuwa mafunzo ya aina hiyo yatasaidia kubadili mawazo na mitazamo ya kiutendaji wa shughuli za vyama vya siasa nchini ili  kujielekeza katika mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa.

Baadhi ya mada zilizowasilishwa wakati wa mafunzo hayo ni jinsi ya kuendesha chama kama taasisi, utaratibu wa kukagua hesabu za fedha za vyama vya siasa na mambo muhimu ambayo vyama vinapaswa kuzingatia.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo ambayo Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini inaendelea kuyatoa kwa vyama vya siasa ili kusaidia vyama hivyo kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na kujiendesha kama taasisi.