Ulinzi na usalama kwa watoto hauridhishi

0
129

Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Juma Kizija amesema hali ya ulinzi na usalama wa wanafunzi wa shule za awali, msingi na Sekondari nchini sio ya kuridhisha sana kwa kuwa bado vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa wanafunzi vinaendelea kufanyika.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya utekelezaji wa mpango wa shule salama katika Manispaa ya Lindi kwenye ukumbi wa mikutano Ngudu, Kizija amekumbusha kwamba watoto anaowazungumzia ni zaidi ya nusu ya Watanzania wote kwani kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, asilimia 50.1 ya watu wote Tanzania ni watoto.

Amesema utafiti uliofanyika nchini unaonesha kwa kila msichana mmoja kati ya watatu na mvulana mmoja kati ya saba wamefanyiwa ukatili wa aina mbalimbali kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na kwamba inakadiriwa asilimia 72 ya wasichana wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili.

Ametaja visababishi vikubwa vya ukatili huo kuwa baadhi ya familia ni watoto kujilea wenyewe, kushindwa kutoa mahitaji ya msingi, walimu kushindwa kutathmini miongozo ya utoaji adhabu kwa wanafunzi, mazingira na miundombinu duni isiyo rafiki shuleni, msongo wa mawazo kwa walimu, umbali wa shule na makazi ya wanafunzi na wazazi kufumbia macho vitendo viovu.

Ameongeza pia kwamba ili mtoto awe salama wadau wa ulinzi na usalama wa mtoto hawana budi kuzingatia mazingira salama ya kuishi, kucheza na kusoma, kuhakikisha ulinzi na usalama wake dhidi ya unyanyasaji kimwili na kisaikolojia, lishe bora, kumpa uhuru wake, kumthamini na kumpatia haki na stahiki zake za kielimu.

Amevitaja viashiria vya unyanyasaji wa mtoto kuwa ni utoro wa mara kwa mara shuleni, mtoto kuwa mwoga bila sababu na kushindwa kujieleza, kurudi nyuma katika maendeleo yake ya kitaaluma, kujitenga na wanafunzi wenzake nyumbani na shuleni pamoja na baadhi ya watoto kuonesha vitendo vya ukatili kwa watoto wenzao.

Semina ya mafunzo ya programu ya shule salama inaendela katika Manispaa ya Lindi ikiwa imejumuisha walimu wa sekondari kutoka mikoa ya Morogoro, Lindi na Dar es Salaam ambao wanatekeleza mpango wa shule salama katika vituo vyao vya kazi.