Ukabila usipewe nafasi – Kinana

0
151

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana amewasisitiza wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kujitenga na tabia ya kukumbatia ukabila, akisema ni mambo ya kizamani, yanayowagawa wananchi.

Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Shirati, Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, leo Aprili 15, 2024 Kinana amesema nchi kuwa na makabila ni jambo la kawaida ila ukabila ni jambo baya, lisilopaswa kupewa nafasi.

Kinana amesema hayo baada ya baadhi ya wajumbe kuibua hoja kwamba kuna mambo yanafanyika katika Wilaya ya Rorya ambayo yanaashiria uwepo wa changamoto ya ukabila.

Ameeleza kwamba Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ametokea kabila dogo mkoani humo, lakini ameongoza nchi kwa miaka 24, na kwamba alipendwa, aliheshimiwa na kuthaminiwa.

“Sasa usimpe mtu nafasi ya uongozi kwa sababu ya kabila lake, dini au umbile. Hayo ni mambo ya kizamani sana. Tumwangalie mtu ana uwezo? Atafanya kazi? Atajituma na kujitolea? Mnampima kwa vigezo sio kwamba huyu ni ndugu yangu,” amesema.

Katika ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti Kinana pia amefika Mwitongo nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambapo alizuuru kaburi lake na kuweka shada la maua.