Ulishapita Shekilango? Mwenye jina hilo wamjua?

0
256

Jijini Dar es Salaam kuna Barabara Mashuhuri inayoitwa ‘Shekilango’, ikianzia maungio ya Barabara ya Morogoro, eneo la nyumba za NHC, mkabala na Kiwanda cha Urafiki, ikipitia mitaa yote ya Sinza na kuishia M
maungio ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kituo cha Bamaga.

Ni Watanzania wachache wajuao kuwa barabara hiyo ya Shekilango imepewa jina hilo kwa ajili ya heshima ya Ndugu Hussein Ramadhani Shekilango, aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, akishughulika zaidi na mambo ya Utawala, wakati wa Uongozi wa Rais Julius Nyerere, Makamu wake wa kwanza akiwa Aboud Jumbe Mwinyi.

UBUNGE KOROGWE HADI UWAZIRI

Hussein Shekilango alichaguliwa na wananchi wa kwao kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Jimbo la Korogwe Mjini, mkoani Tanga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1975, akiachia nafasi yake ya zamani ya Meneja Mkuu wa Shirika la Usagishaji la Taifa (National Milling Corporation).

Mwaka huohuo, akachaguliwa na Rais Nyerere kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Utawala) akiwa chini ya Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu, Ndugu Rashid Mfaume Kawawa.

Mwaka 1977 yalifanyika mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri nchini. Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Edward Moringe Sokoine akateuliwa kuwa Waziri Mkuu akichukua nafasi ya Kawawa. Shekilango akabakishwa katika nafasi yake lakini akiwa na bosi mpya.

VITA VYA UGANDA

Mara baada ya mapambano ya Vita vya Kagera, mwaka 1979 vikosi vya Jeshi la la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vilifanikiwa kumng’oa madarakani Dikteta Idd Amin wa Uganda na Ndugu Yusufu Lule akawa Rais wa mpito wa taifa hilo jirani.

Lule hakudumu sana madarakani kwani mwezi Juni, 1979 naye aling’olewa madarakani kwa kutofautiana na Baraza la Ushauri la Taifa la nchi hiyo juu ya uteuzi wa nafasi za mawaziri. Nafasi yake ikachukuliwa na Ngudu Godfrey Binaisa.

KUPELEKWA UGANDA

Miezi kadhaa baada ya Binaisa kuchukua madaraka katika Serikali ya Uganda bado mambo ya kuendesha nchi hiyo hayakuonekana kwenda vizuri. Changamoto za kujenga upya nchi hiyo iliyoharibiwa na vita zilikuwa kubwa, huku jeshi jipya la nchi hiyo likiwa na kashfa ya kufanya ukatili kwa wananchi na pia kushiriki kwenye uhalifu na uporaji.

Ili kuimarisha mambo ya kiutawala ya nchi hiyo ilimbidi Rais Nyerere ambaye bado vikosi vya jeshi la Tanzania vilikuwa havijaondoka Uganda, ampeleke Waziri Shekilango kwenda kusaidia mambo ya kiutawala ya nchi hiyo na kuwa mratibu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uganda.

Mwezi Mei, 1980 ilizuka sintofahamu kubwa katika Utawala wa Uganda, Rais Godfrey Binaisa alimwondoa jeshini Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo (zamani akiitwa Chief of Staff), David Oyite Ojok na kumteua kuwa Balozi wa Uganda nchini Algeria, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni nidhamu mbaya ya jeshi la nchi hiyo hasa kwenye masuala ya ukatili kwa wananchi na uporaji.

Uamuzi huo wa Rais Binaisa haukumfurahisha kiongozi huyo namba mbili wa Jeshi la nchi hiyo, hivyo alikataa uteuzi mpya, na wanajeshi waliokuwa watiifu kwake wakatangaza kumuunga mkono na kupanga mikakati ya kumwondoa madarakani Rais Binaisa aliyekuwa akilindwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Kasri la Rais la Entebbe.

Misururu mirefu ya magari ikaonekana katika Jiji la Kampala, ambapo wanajeshi watiifu kwa David Ojok walikuwa wakiyapekuwa magari yote yaliyokuwa yakitoka na kuingia ndani ya jiji hilo ili kuhakikisha hakuna silaha, huku pia wakikiteka Kituo cha Redio cha Taifa cha nchi hiyo.

Wanajeshi wafuasi wa Ojok waliweka vizuizi katika barabara zote za Jiji la Kampala na kuamua kuyalinda majengo yote nyeti ya Serikali likiwemo jengo la Nile Mansion Hotel ambalo ndilo lililokuwa na ofisi nyingi za wizara nyeti za Serikali ya nchi hiyo.

Kung’olewa kwa Binaisa kulifanywa na Tume maalumu ya watu sita, ambayo ilikuwa ni sehemu ya Baraza la Ushauri la Taifa lililomng’oa Rais Lule, huku matendo ya Tume hiyo pamoja na Ojok kwenye wiki hiyo yakihusishwa zaidi na Rais Milton Obote aliyekuwa ughaibuni, ambaye aling’olewa madarakani na Amin mwaka 1971. Obote alikanusha kuhusika na matendo hayo ya Ojok yaliyokuwa yakiteteresha hali ya ustawi wa nchi hiyo japo haikubadili ukweli kuwa marafiki hao lao lilikuwa moja.

WAZIRI SHEKILANGO KULETA TAARIFA

Katika hali ya matatizo yote hayo, Waziri Hussein Ramadhani Shekilango pamoja na Balozi Kilumanga waliamua kupanda ndege kwenda kumpa habari za namna hali halisi ya mambo ilivyo nchini humo Rais Nyerere ambaye alikuwa kwenye ziara ya kiserikali mkoani Arusha. Safari hiyo ndiyo ikawa mwisho wa maisha yao.

Ilikuwa siku ya huzuni mno kwa kumpoteza Waziri huyo damu changa, tarehe 11 Mei, 1980. Ndege ya kijeshi iliyowachukua Shekilango, Balozi Kilumanga pamoja na wanajeshi wanne wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ilianguka katika vilima vya Jiji la Arusha na abiria wote kupoteza maisha, wakiacha huzuni na majonzi mazito kwa Watanzania.

Msafara wa Rais ukakatisha ziara na shughuli ya mapokezi ya miili ya mashujaa wetu hao ndiyo ikawa ratiba rasmi, huku Rais Nyerere akionesha kwa dhati namna alivyohuzunishwa kwa kumpoteza waziri huyo mchapa kazi kwa Taifa.

Majonzi zaidi yakiwa kwa Wananchi wa Korogwe waliopoteza kijana wao, msomi wa Makerere aliyejitolea kuwatumikia kwa dhati, Shekilango.

Shujaa huyu alizikwa kijijini kwao Jitengeni, Korogwe, Mkoani Tanga, huku akisindikizwa na umati mkubwa wa watu, mpaka leo akibaki mbunge kipenzi cha watu kuwahi kutokea Korogwe na akisifika Serikalini kwa hatua yake ya kurudisha madaraka mikoani. Kwa kumuenzi kuna shule yenye jina lake Jimboni Korogwe.

Mamlaka za uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kutambua mchango wa Shekilango kwa Taifa, ikaamua kuipa barabara mpya iliyokuwa inajengwa wakati huo jina la Shekilango ili kumuenzi shujaa huyu.

MKE NA WATOTO

Marehemu Shekilango, aliyekuwa “amekwenda hewani” aliacha watoto ambao walikuwa wakifahamika kwa urahisi kutokana na urefu wao, pamoja na mkewe Mama Zappora. Marehemu Shikilango alikuwa akiishi Sea View, Dar es Salaam kwa muda mrefu na baadae familia yake ikahamia kwenye nyumba yao iliyopo Kinondoni Bwawani.

Mama Zappora aliyezaliwa mwaka 1938 alikuwa ni mwalimu hodari sana na amefundisha shule nyingi hapa nchini. Aidha, alikuwa “Headmistress” shule za wasichana Zanaki, Kisutu, Jangwani, Forodhani, Msalato na Iringa Girls Secondary School. Mama Zappora, ambaye ni mmoja wa ma-headmistress walioweka rekodi ya kuongoza shule nyingi nchini, alifariki tarehe 1.9.2018. Licha ya marehemu Shekilango kufariki, lakini mwanamke huyu ngangari aliweza kuwalea wanae vizuri.

CHANZO: Mitandao na vyanzo mbalimbali