Uchafuzi wa mazingira watajwa kuongeza ukinzani wa dawa

0
175

Utafiti mpya umefichua uhusiano kati ya uchafuzi wa mazingira na ukinzani wa dawa katika mwili wa binadamu, jambo ambalo limeelezwa kuwa tishio kwa afya ya binadamu.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la ‘Lancet Planetary Health’ umehusisha ukusanyaji wa data kutoka kwa nchi zaidi ya mia moja kwa kipindi cha takribani miaka 20.

Utafiti huo umegundua kuwa viwango vya juu vya uchafuzi wa hewa vinahusishwa na viwango vya juu vya ukinzani wa antibiotiki mwilini yani bakteria kuwa sugu kwa dawa ambazo hutumika kwa matibabu kwa binadamu ambapo kadiri uchafuzi huo unavyoongezeka ndivyo ukinzani unavyoongezeka pia.

Hata hivyo watafiti kutoka China na Uingereza wameeleza kuwa utafiti huo ni uchambuzi wa awali wa kimataifa wa namna uchafuzi wa hewa unavyoweza kusababisha antibiotiki kushindwa kutibu mwili wa binadamu.

Ingawa sababu kuu ya ukinzani wa antibiotiki mwilini mwa binadamu ni matumizi mabaya au matumizi ya kupita kiasi ya antibiotiki, lakini utafiti huo unabainisha uchafuzi wa hewa hufanya tatizo kuwa kubwa zaidi kwani bakteria hutengeneza genes [jeni] zinazowafanya kuwa na kinga dhidi ya dawa za antibiotiki hivyo kupelekea magonjwa yasiyotibika.