TASAC : Boti imezama wakati wa majaribio

0
698

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa taarifa kuhusu tukio la kuzama kwa boti ya uvuvi yq MV LEGACY na kusema kuwa ilizama ikiwa katika majaribio ya kiufundi baada ya matengenezo ya mifumo ya uvuaji samaki kwa kukokota.

Taarifa ya TASAC iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa boti hiyo iliyozama Machi 10, 2024 majira ya alasiri ilianza majaribio majira ya saa tatu asubuhi ikitokea maeneo ya Tandavamba, Kivukoni na kufanya majaribio ya kuvua samaki kuzunguka katika maeneo yenye maji mafupi karibu na eneo la daraja jipya la Tanzanite hadi Coco Beach.

Ilipofika saa 9:50 Alasiri wakati nahodha anabadilisha uelekeo wa boti kuelekea upande wa kulia ndipo kamba moja ya upande wa kushoto ilikatika na kusababisha uzito kuelemea kwenye kamba ya upande wa kulia na ndipo uzito ulipohama ghafla na kuilazimisha boti kunywa maji upande wa kulia kisha kuzama.

Boti hiyo ya uvuvi ya MV LEGACY inamilikiwa na Yakoub Juma Khamis na ilipatiwa cheti cha usajili na ubora na TASAC kufanya shughuli za uvuvi Machi 06, 2024.

Wakati ajali hiyo inatokea boti hiyo ilikuwa na mabaharia tisa ikijumuisha wavuvi sita, mhandisi mitambo mmoja na manahodha wawili na wote wameokolewa na wanaendelea vizuri kiafya.