Simiyu yanufaika Miaka Mitatu ya Rais Samia

0
215

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuufungua Mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza miradi mikubwa mitano ya kitaifa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja.

Meneja wa TANROADS mkoani Simiyu, Boniface Mkumbo ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi ambapo wamefanikiwa kukamilisha ujenzi wa awamu ya tatu ya kipande cha barabara ya Bariadi – Maswa yenye urefu wa Km 49.7 pamoja na barabara ya mchepuo ya Maswa ( Maswa Bypass) sehemu ya Lamadi – Bariadi – Maswa – Wigelekelo hadi Mwigumbi upande wa Shinyanga na daraja la Malampaka lenye mita 12.5.

Amesema miradi mingine mitatu ya zaidi ya kilomita 300 ipo kwenye utekelezaji wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami ambapo pia wamejenga madaraja zaidi ya 20 kwa gharama ya shilingi Bilioni 5.6.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu cha Serikali ya awamu ya sita zaidi ya taa 569 za barabarani zimefungwa kwenye miji na vijiji vikubwa ili kuwafanya wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii hata giza linapoingia.

Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwajali Wakandarasi Wazawa ambapo Mkoa wa Simiyu ni moja kati ya mikoa ambayo kazi nyingi wamepewa Wakandarasi wa ndani na kuwapa Kipaumbele Wanawake ili kuweza kuwawezasha kupewa upendeleo na hivyo kuwakuza kiuchumi.